*****************************************
(Na Jovina Bujulu-MAELEZO)
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususan ile ya kimkakati na inayolenga kuboresha huduma pamoja na maisha ya wananchi na kuhakikisha kuwa inakuwa na viwango vinavyoendana na thamani ya fedha za walipa kodi.
Aliyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2021/22.
Aidha, alisema kuwa Serikali itaimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha za umma sambamba na uwajibikaji ikiwa ni pamoja na kutumia rasilimali chache zilizopo katika shughuli za uzalishaji mali na kuongeza tija ili kuchochea ukuaji wa haraka wa uchumi na maendeleo ya watu.
Aliitaja baadhi ya miradi inayoendelea kutekelezwa kuwa ni pamoja na Ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR), ambayo ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 90.34, na kipande cha Morogoro – Makutopora (km 422) umefikia asilimia 57.57 na tayari Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa kipande cha Mwanza – Isaka (km 341) wenye thamani ya shilingi trilioni 3.07.
Miradi mingine ni mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (Megawati 2,115) ambapo utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 45 hadi Machi 2021. Mradi huo mpaka sasa umetumia jumla ya shilingi trilioni 2.1 na kuzalisha ajira zaidi ya 7,000.
Kwa upande wa mradi wa usambazaji umeme vijijini, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kuwa hadi Februari 2021, jumla ya vijiji 10,294 kati ya vijiji 12,317 sawa na asilimia 83.3 vilikuwa vimeunganishwa umeme kupitia mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini na Makao Makuu ya Wilaya (REA III). Mradi huo umekwisha tumia shilingi bilioni 323.7.
Alibainisha kuwa faida za kufikisha umeme katika vijiji hivyo ni pamoja na maeneo husika kuimarika na kukua kwa biashara za wananchi na hivyo kujiongezea kipato. Aliongeza kuwa lengo la Serikali ni kukamilisha usambazaji umeme katika vijiji vyote hadi visiwani na kwenye vitongoji.
Kuhusu huduma za usafiri na usafirishaji kwenye maziwa makuu, alisema kuwa kwa upande wa Ziwa Victoria, Serikali imejenga chelezo na meli mpya ya MV Mwanza ‘Hapa Kazi Tu’ pamoja na kukarabati meli za New Butiama, New Victoria, MV Clarias na ML Wimbi, ambapo katika Ziwa Tanganyika Serikali inaendelea na ukarabati wa meli za MV Liemba na MT Sangara pamoja na kukamilika kwa mikataba kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo.
Aidha, Serikali imekamilisha ujenzi wa matishari mawili yenye uwezo wa kubeba tani 1,000 kila moja pamoja na kukamilika na kuanza kufanya kazi kwa meli mpya ya MV Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200.
Miradi mingine iliyokamilika ni pamoja na barabara ya juu ya Kijazi iliyopo jijini Dar es Salaam ambayo ilizinduliwa na Hayati Dkt. Magufuli na ujenzi wa daraja la Kigongo- Busisi lililopo Mwanza unaendelea na umefikia asilimia 14.5 na daraja la Tanzanite lililopo jijini Dar es Salaam unaendelea ambapo umefikia asilimia 71.3.
Kwa upande wa miradi ya maji, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kuwa wastani wa watu wanaopata huduma ya maji safi na salama imefikia asilimia 86 mijini na asilimia 72 vijijini ambapo hadi kufikia Machi, 2021 shilingi bilioni 241.3 zimekwisha tumika na kazi ya usambazaji maji vijijini inaendelea.
Katika Sekta ya elimu, Serikali imejenga na kukarabati miundombinu muhimu katika shule za msingi, sekondari na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ambapo jumla ya shilingi bilioni 178 zimetumika kufikia Machi 2021. “ Uimarishaji wa miundombinu ya elimu utasaidia kuongeza ubora wa elimu inayotolewa na hivyo kuongeza idadi ya wahitimu wanaoweza kuajiriwa na kujiajiri”, ameongeza Majaliwa.
Katika kuimarisha sekta ya afya Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 69.4 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwa kujenga na kukarabati miundombinu ya afya inayohusisha hospitali za rufaa za kanda, mikoa, na hospitali za halmashauri ikiwa ni pamoja na kujenga vituo vya afya na zahanati nchi nzima. Hatua zote hizo zimewawezesha wananchi wengi kupata huduma ikiwa ni pamoja na kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.
“ Serikali itahakikisha ahadi alizotoa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan na aliyekuwa Rais wetu, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli zinatekelezwa sambamba na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020”, alisema Waziri Mkuu Majaliwa.