Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela akizungumza kwenye uzinduzi huo
Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela akiangalia mtambo wa kisasa wa kuchanganya rangi za magari.
Mkurugenzi wa kampuni ya Masari Investment Mohamed Saleh Abri akizungumza wakati wa uzinduzi wa duka kubwa la kisasa la kuuza Rangi la Masari liloko manispaa ya Iringa
*************************
NA DENIS MLOWE,IRINGA
WAFANYABIASHARA nchini wametakiwa kuondokana na hofu ya kuwekeza kwa sasa kutokana na Serikali kuweka mfumo mzuri wa wafanyabiashara kufanya biashara zao bila usumbufu wowote kuweza kuongeza ajira na ukusanyaji wa kodi.
Hayo yamesemwa na mmoja ya Wakurugenzi wa Masari Investment, Mohamed Salehe Abri wakati wa uzinduzi wa duka la kuuza rangi za aina mbalimbali uliofanyika hivi karibuni mkoani Iringa na kuzinduliwa na mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela.
Alisema kuwa serikali iliyochini ya rais Mama Samia Hassan Suluhu imeweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara kufanya shughuli zao bila vikwazo hali ambayo inafanya wafanyabiashara wengi kuanza kurudisha imani kwa serikali.
Alisema kuwa awali kulikuwa hofu kwa wafanyabiashara kufunga biashara zao kutokana na kodi lakini mara baada ya tamko la Rais Suluhu kuhusu masuala ya kodi wafanyabiashara wengi wameanza kufungua biashara mbalimbali ikiwemo kampuni ya Masari kufungua duka kubwa la kisasa kuuza rangi mbalimbali za magari na nyumba.
Abri aliishukuru serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa moyo na kuwafariji wafanyabiashara wote na kutoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji waelewe kuwa nyumbani kumenoga na wasisite kufanya biashara.
“Serikali hii ni serikali rafiki kwa wafanyabiashara, imetuunga mkono na sisi kama wafanyabiashara tutaiunga mkono kwa kulipa kodi na kuhakikisha kwamba nchi yetu tunaisogeza mbele pale inapotakiwa kuwepo” alisema
Kwa upande wake mgeni rasmi katika uzinduzi huo wa duka jipya la Masari Invesrment, mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela kuwa Rais Mama Samia baada ya kauli yake kwa TRA wafanyabiashara wengi wameanza kufungua biashara mbalimbali kwa kuwa na imani na serikali yao.
Alisema kuwa kampuni ya Masari waliandaa duka hili kwa muda mrefu sana takribani miaka minne lakini walikata tamaa na baada ya kauli ya rais Mama Samia wamejitokeza na kufungua mapema na kuna kiwanda kipya kinatarajiwa kufunguliwa kutokana na kauli za rais kuwa rafiki kwa wafanyabiashara.
Alisema kuwa alipigiwa simu na wanaotaka kufungua viwanda hivyo na kusema kuwa walimwambia’ huu ndio wakati mwafaka wa kufungua biashara ikiwa na maana kwamba mioyo imeanza kufunguka kwani inawezekana wakusanya kodi hawakujua kwamba wanaumiza hawa wananchi.
“Wengi wa wakusanya kodi walikuwa wanafungia watu hali ambayo ilileta sintafahamu kwa wafanyabiashara wengi hivyo kauli ya mama kwamba kodi ikusanywe lakini sio kwa kuwadhurumu watu imesaidia sana kwa wafanyabiashara kuanza kufungua biashara zao na kuwashukuru Masari kwa kuonyesha njia kwani ufunguzi huo utaleta ajira kwa vijana” alisema
Alisema kuwa licha ya kuzalisha ajira Masari wamekubali kutoa mafunzo kwa vijana mia moja kwa ajili ya kupata elimu ya kuchanganya rangi kutoka kwa wataalam hali ambayo itaongeza idadi ya ajira kwa watakaopata mafunzo kufanyia kazi elimu hiyo.