*********************************
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Jaji mkuu wa mahakama ya Tanzania Profesa Ibrahim Juma amesema kuwa mahakama inajitahidi kuhakikisha inafanya shughuli za ujenzi ili kuondoa changamoto za miundo ya mahakama na kuweza kufikisha huduma katika mikoa na wilaya zote nchini.
Profesa Ibrahim Juma Ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa time ya utumishi wa mahakama na wajumbe wa kamati za maadili za mkoa wa Arusha ambapo alisema kuwa mahakama ina changamoto ya miundombinu ambapo wamepata nafasi ya kuboresha mpango mkakati wa kuboresha miundombinu na wanapokea maoni na mawazo ya wadau kuhusu maeneo yenye changamoto ya ujenzi.
Amesema kuwa katika Kikao hicho lengo kubwa lililowaleta ni maadili kutokana na tathimini inayoonyesha kwamba wananchi wengi hawafahamu vema majukumu ya tume na kamati za maadili kwani wamekuwa wakiwasilisha malalamiko ambayo tayari yanatakiwa yashughulikiwe na mifumo ya kimahakama.
“Kwahiyo nyinyi wajumbe mkiweza kufahamu mipaka ya kazi zenu mnakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuwaelimisha wananchi waelewe masuala ya nidhamu yakoje na yakimahama yakoje,” Alisema Profesa Ibrahim.
Ameeleza kuwa tume ya utumishi wa mahakama kwa mujibu wa katiba ina jukumu la kusimamia mahakama katika masuala ya rasilimali watu, rasilimali fedha, miradi pamoja na jinsi inavyotoa za utoaji haki.
“Ili kujiridhisha na utendaji uliotajwa tume imeona kuna umuhimu wa kufanya ziara ili kuona hali halisi ya utekelezaji wa majukumu ya mahakama ili kuipa uelewa katika kufanya maamuzi,”Alisema Jaji Profesa Ibrahim.
Kwa upande wake Jaji mfawidhi wa mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma Ilvin Mugeta alisema kuwa majukumu ya kamati ni kupokea na kuchunguza malalamiko dhidi ya jaji wa mahakama ya rufani, jaji kiongozi au jaji wa mahakama kuu ambapo ya kupokea wanatakiwa kuwasilisha kwamajaji hao malalamiko yaliyotolewa.
Jaji Mugeta alifafanua kuwa kamati hizo pia zinatakiwa kuwasilisha Kwa time malalamiko hayo, kusikiliza, kumuonya pamoja na kuchukua hatua yoyote Ile ambayo itafaa kulingana na mazingira.
Naye mkuu wa mkoa wa Arusha Iddi Kimanta ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo ngazi ya mkoa alisema kuwa kutoka na geografia ya mkoa huo wananchi wanatembea umbali mrefu kufikisha huduma za kimahakama hivyo ameiomba mahakama kuangalia namna ambayo wananchi watapata huduma Kwa urahisi.