…………………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Serikali imesema kuwa itahakikisha inazingatia maslahi ya watumishi wa Umma ikiwemo nyongeza ya mishahara, malipo ya wastaafu na kupandiswa kwa madaraja kwa mujibu wa sheria huku inakusudia kutangaza ajira mpya zipatazo 40,731.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Mohammed Mchengerwa wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi Katika Utumishi wa Umma uliofanyika leo April 14,2021 jijini Dodoma.
Mhe.Mchengerwa amesema kuwa masuala kama nyongeza ya mishara, kupandishwa kwa madaraja ya watumishi, malipo ya wastafu ni mambo ambayo yapo kwa mujibu wa sheria hivyo utekelezaji wake ni wa lazima na siyo hiyari.
“Mtumishi kuongezwa mshahara, kupandishwa madara au kupandishwa vyeo haya yapo kwa mujibu wa sheria na siyo ombi wala huruma ya mwajiri wake hivyo tutahakikisha kuwa tunatekeleza kwa mujibu wa sheria inavyo elekeza”amesema Mchengerwa
Aidha Waziri Mchengerwa amesema kuwa Serikali inakusudia kutangaza ajira mpya zipatazo 40,731 katika sekta za kipaumbele na zenye changamoto za uhaba wa watumishi hizo ni tofauti na zile 6,000 za kada ya ualimu na 2,000 za afya ambazo zenyewe zilishatangazwa.
Mchengerwa amesema kipaumbele katika ajira hizo mpya ambazo zitatangazwa kitakua katika sekta ya elimu kwa maana ya walimu wa masomo ya sayansi, hisabati na kiingereza, sekta ya afya kwa maana ya madaktari na wauguzi pamoja na sekta ya kilimo.
” Huu ni mpango wa Serikali inayoongozwa na Rais wetu Samia Suluhu Hassan, lengo letu tunafahamu kuwepo kwa changamoto ya ajira nchini lakini kwa kuanza tutatangaza hizo chache, niwaahidi watanzania kwamba serikali itaendelea kuweka bajeti ya kuhakikisha kila mwaka kunakua na ajira mpya.
Kama serikali tumepanga kuwashika mkono watanzania lakini pia tumepanga kuwashika mkono watumishi wake wote, niwaombe tu wazidi kuchapa kazi kwa uzalendo, uadilifu na nidhamu huku wakisimamia maadili na taratibu zote za utumishi wa umma,” Amesema Waziri Mchengerwa.
Amewataka waajiri na watumishi wote wa umma nchini kuacha matumizi ya mabavu, uonevu na ubabe na badala yake wajikite kuwahudumia watanzania kwani serikali ya Rais Samia inaamini inaweza kufanikiwa bila kutumia nguvu.
Katika mkutano huo wa Baraza la wafanyakazi, Waziri Mchengerwa amesisitiza ushirikishwaji wa watumishi katika maamuzi kwani jukumu la wafanyakazi kushirikishwa ni suala la kikatiba na liliwahi kusisitizwa na hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
” Nitoe rai kwa Viongozi mliohudhuria baraza hili kuacha kufanya maamuzi bila kuwashirikisha watumishi wetu, niagize kwenu waajiri wote kuhakikisha mabaraza yote ya Wafanyakazi yanakua hai na katika mkutano ujao nipewe taarifa ya mabaraza yote, lengo ni kuangalia namna gani Wafanyakazi wetu wanashirikishwa katika maamuzi,” Amesema Mchengerwa.