……………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
MBUNGE wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota ameomba Wizara ya Kilimo kushughulikia kero zilizojitokeza katika mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuendelee kuleta mafanikio zaidi kwenye sekta ya korosho.
Pia, ameishauri serikali kuanza kutekeleza mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma na Liganga ili Bandari ya Mtwara ilifanye kazi kwa ufanisi.
Akichangia leo bungeni bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2021/22, Chikota amesema zao la korosho tangu mwaka 2004 hadi 2017, kumekuwepo na ongezeko la uzalishaji wa korosho, na imetokana na uwekezaji mkubwa uliowekwa na serikali katika zao hilo.
“Mwaka 2004 tulikuwa na tani 72,000 na mwaka 2017 tulifikisha tani zaidi ya 300,000 za korosho, kulikuwa na uwekezaji mkubwa ndio maana tulifanikiwa kwa kiasi hicho,”amesema.
Amefafanua kuwa kuanzia 2008 kuna kushuka kwa uzalishaji wa korosho kwasababu ya kupunguzwa fedha katika sekta ya korosho.
“Nimpongeze Waziri wa Kilimo kwa jitihada wanazozichukua hivi sasa kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wakulima ili uzalishaji uanze kuongezeka hongereni sana.”
“Lakini nizungumzie soko la korosho hotuba ya Waziri Mkuu ameweka kinagaubaga kuwa ushirika utaendelezwa lakini vile mauzo kwa mazao ya kimkakati utaendelea kuwa chini ya minada chini ya mfumo wa stakabadhi ghalani,”amesema
Ameomba Wizara ya Kilimo kurekebisha dosari zilizopo lakini mfumo huo umeleta mafanikio makubwa sana kwenye sekta ya korosho.
“Naomba tuulinde ili wakulima wanufaike na korosho… TMX iendelee na masoko ya nje maana kwa masoko ya ndani imeonekana ni changamoto ambazo hazijapatiwa kwenye ufumbuzi,”amesema.
Pia amehimiza matumizi ya bandari ya Mtwara kutokana na serikali kufanya uwekezaji mkubwa uliogharimu zaidi ya Sh.Bilioni 57.