********************************
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika Manispaa ya Songea (SOUWASA) ni moja ya taasisi za Serikali zilizo chini ya Wizara ya Maji.
Hata hivyo kulingana na takwimu za SOUWASA, ni watu 216,706, sawa na asilimia 86.2 ndiyo kwa sasa wanapata huduma ya maji safi na salama.
Mkurugenzi Mtendaji wa SOUWASA, Mhandisi Patrick Kibasa anasema Songea inapata maji kutoka vyanzo vya maji vilivyopo katika Bonde la Ziwa Nyasa pamoja na Bonde la Mto Ruvuma.
Anataja vyanzo vilivyopo katika Bonde la Mto Ruvuma na Pwani ya Kusini kuwa ni Ruvuma, Lipasi, Liwoyowoyo, Lihwena, Lilambo na Likuyufusi ambavyo huzalisha meta za ujazo 12,300 kwa siku.
“Kwa sasa mahitaji ya maji ni wastani wa meta za ujazo 25,862 katika maeneo yote ya Manispaa’’,anasisitiza.
Kibasa anasema mamlaka hiyo ina mtambo wa kusafisha na kutibu maji safi, ujazo wa meta 11,500 kwa siku, matanki 10 yenye ujazo wa meta 4,490 kati ya mahitaji ya meta za ujazo 10,000 na mtandao wa mabomba ya maji safi wenye urefu wa km 495.8.
Akizungumzia mtandao wa maji taka Kibasa anasema, kwa jumla mtandao wa mabomba ya maji taka una urefu wa km 37.7 pamoja na mtambo wenye uwezo wa kusafisha na kutibu majitaka meta za ujazo 2,100 kwa siku.
Hata hivyo anasema, hadi sasa idadi ya wateja wa maji safi ni 18,940 na wateja wa maji taka 1,497 huku kiwango cha maji yanayopotea ukiwa asilimia 22.
Kuhusu mafanikio ya SOUWASA,Mhandisi Kibasa anasema SOUWASA imepata mafanikio makubwa ikiwemo kuongeza idadi ya watu wanaopata huduma ya maji safi kutoka 142,246 Juni 2015 hadi kufikiwa 216,706 mpaka Februari 2021.
Mafanikio mengine ni kuongeza kiwango cha huduma ya usambazaji maji safi kutoka asilimia 74 hadi 86.2 ya wakazi wa kata za mjini na kuongezeka kwa mtandao wa mabomba ya usambazaji maji safi kutoka km 330.59 hadi km 495.837.
Kibasa anasema pia SOUWASA imefanikiwa kuimarisha uhifadhi wa mazingira katika Bonde la Luhira na kuongezeka kwa idadi ya wateja wa huduma ya maji safi kutoka 12,256 hadi 18,940 na wale wa maji taka kuongezeka kutoka 1,179 hadi 1,497.
Licha ya mafanikio hayo anazitaja changamoto kubwa ni Manispaa ya Songea kuwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu kwa sababu ni miongoni mwa miji inayokua kwa kasi Tanzania.
Hali hiyo anasema imesababisha vyanzo vya maji vilivyopo kutotosheleza, hivyo baadhi ya maeneo kutofikiwa na mtandao wa mabomba ya maji.
Changamoto nyingine anazitaja kuwa ni uchomaji moto hovyo na shughuli za kilimo kufanyika katika maeneo ya vyanzo vya maji na kuathiri upatikanaji wa maji.
Ili kukabiliana na changamoto hizo anaitaja
mikakati itakayosaidia kutatua changamoto hizo kuwa ni kuendelea kutumia fedha za ndani kufanya uwekezaji mdogo wa miundombinu ya maji safi ili kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma na kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira katika vyanzo vya maji.
Hata hivyo anautaja Mji wa Songea ni miongoni mwa miji 28 nchini itakayonufaika na mradi wa maji kupitia ufadhili wa Serikali ya India utakaogharimu Dola za Marekani 45,315,701.00.
Anasema fedha hizo zitasaidia kupanua mtandao wa maji na kuboresha huduma na kwamba mradi huo utahusisha ujenzi wa bwawa la kuhifadhia maji, upanuzi wa mtambo wa kusafishia na kutibu maji safi lita 51,459,000 kwa siku.
Kibasa anasema fedha hizo, zitasaidia kujenga matangi manne ya kuhifadhia maji yenye uwezo wa kubeba lita 18,200,000 na ulazaji wa mabomba ya kusafirisha na kusambaza maji yenye urefu wa km 190.3.
Kwa mujibu wa Kibasa Mamlaka hiyo pia imepewa maelekezo na Wizara ya Maji kuzilea mamlaka ndogo mbili za Tunduru na Mbinga ili kuzijengea uwezo kabla ya kujiendesha zenyewe.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SOUWASA, Dkt. Anslem Tarimo, anasema,siku za nyuma hali ya utoaji huduma ya maji haikuwa nzuri kwa sababu ni watu wachache wanaoishi katika eneo la mji wa Songea waliokuwa wanapata huduma ya maji safi.
Dk Tarimo anasema, hivi sasa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa Manispaa ya Songea inaridhisha na kuwapongeza watendaji wa SOUWASA kwa kazi nzuri.
SOUWASA ilianzishwa mwaka 1997 kwa ajili ya kutoa huduma zake za maji katika Manispaa ya Songea inayokadiriwa kuwa na wakazi 299,543.