……………………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
BUNGE limeelezwa kuwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ilisitisha mafunzo ya vijana wa kujitolea MF 2020/21 kutokana na kutoa nafasi kwa JKT kutathmini mafunzo yaliyofanyika na kuandaa utaratibu wa kuwa na mitaala bora ya mafunzo ya Vijana itakayowawezesha Vijana hao kujitegemea wanapomaliza mafunzo badala ya kutegemea kuajiriwa.
Kauli hiyo ametolewa leo Bungeni na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Elias John Kwandikwa wakati alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Wingwi Issa Omary (CCM).
Katika swali lake Mbunge huyo alisema Je, ni kwa nini Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) imewarudisha nyumbani vijana ambao walishafika kambini kwa ajili ya kuanza mafunzo?
Akitaja sababu nyingine Kwandikwa amesema kuwa JKT kwa kushirikiana na Wizara ya Ulinzi na JKT kufanya mawasiliano na Taasisi zingine kama, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, na Tume ya vyuo vikuu (TCU) na Baraza la Mitihani (NECTA) kuandaa utaratibu wa kuongeza muda wa mafunzo ya Vijana wa Mujibu wa Sheria kuwa mwaka mmoja badala ya miezi mitatu ya sasa na kuchukua Vijana wengi zaidi wanaomaliza kidato cha sita huku idadi ya Vijana wa kujitolea ikipunguzwa.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni kutoa fursa kwa JKT kukamilisha mpango wa kuwawezesha Vijana kupata mitaji wanapohitimu mafunzo kwa kushirikisha Taasisi nyingine ambazo ni Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Kazi na Vijana na TAMISEMI.
“ Utekelezaji wa Mkakati huu unasimamiwa na Wizara ya Ulinzi na JKT”alisema.
Aidha amesema kuwa JKT litaendelea kutoa elimu kwa Umma na kwa Vijana wanaojiunga na JKT kujitolea kuelewa kuwa lengo la mafunzo ni kuwawezesha waweze kujitegemea baada ya mafunzo hayo badala ya kutegemea ajira.