******************************
Shirika la CEDESOTA chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS) limefanikiwa kuendesha mradi ujulikanao kama Haki ya Mwanamke kumiliki ardhi, ambao unafanyika katika kata sita za wilaya ya Arumeru ambazo ni Leguruki, King’ori na Malula nyingine ni kata za Marori, Makiba na Mbugani ambazo kwa pamoja zina jumla ya vijiji 26.
Mkurugenzi Mkuu wa CEDESOTA Bw. Jackson Muro anasema lengo kubwa la mradi ni kutoa elimu kwa jamii ya wameru na hasa wanawake ili watambue haki zao katika kumiliki ardhi huku wakiwasaidia kupata hati za umiliki wa ardhi za kimila.
“Tunaendesha mikutano mbalimbali na midahalo ambayo inawakutanisha wanawake kutoka kata sita za mradi , na hapa wanakutanishwa na wanake waliofanikiwa kumiliki ardhi ili wajifunze kutoka kwao, pia wanapewa mafunzo mbalimbali ya namna ya kutetea haki zao na pia kuwatetea wengine katika jamii zao’’
‘’kabla ya mafunzo na elimu kutolewa, wanawake walibaguliwa katika umiliki wa ardhi katika jamii yetu , na tuliona ni kitu cha kawaida lakini kwa sasa , mafunzo ya CEDESOTA, yametuwezesha kujitambua, na kwa kata yetu ya Maroroni , wanawake 11 wanamiliki ardhi’’ anasema mmoja wa viongozi wa kimila bw. Frank Kaaya.
“Baadhi ya viongozi wetu wa kimila kwa sasa wamegundua kwamba mmiliki wa ardhi ni Serikali hivyo mgogoro wowote wa ardhi Serikali ndio mwenye kauli ya mwisho juu ya matumizi sahihi na ya halali ya ardhi hapa nchini” ameongeza Bw. Kaaya.
Bi NDEKUSURA URIO ambaye ni mwenyeketi wa kata ya Kimororoni, ni miongoni mwa wanawake waliopata mafunzo kupitia mradi unaoendeshwa na CEDESOTA.
“Katika kata yangu tayari wanawake nane wamepeleka maombi ya kupata hati ya kumiliki ardhi, saba wamepata ardhi na wengine 10 wanajenga nyumba, kama moja ya matumizi ya kiuchumi ya ardhi hiyo. mradi huu umetusaidia’’
Lilian Pallangyo ambaye ni mnufaika wa mradi huu anasema mafunzo hayo yamewezesha kuwepo kwa majukwaa ya wanawake katika kila kijiji na kwamba kupitia majukwaa hayo wanawezeshwa kukutana na kujadiliana mambo mbalimbali ikiwemo masuala ya uwezeshwaji kiuchumi kupitia ardhi.
licha ya mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi huu, mkurugenzi wa CEDESOTA ,Jackosn Muro anabainisha baadhi ya changamoto ambazo wamekutana nazo wakati wakitekeleza mradi kuwa ni pamoja na:
* Mila na Desturi za jamii hiyo na hivyo ilikuwa ngumu kuishawishi jamii hiyo kubadilika
* wanawake wengi hawakuwa tayari kupokea elimu hiyo
* Uelewa duni kwa viongozi wa jamii na wale wakimila juu ya masuala ya haki sawa kwa mwanamke na mwanaume katika kumiliki mali ikiwemo ardhi .
* kuongezeka kwa migogoro ya ardhi baada ya watu kupata elimu
changamoto nyingine ni gharama kubwa za upatikanaji wa hati za kumiliki ardhi na hivyo kuwafanya wanawake wengi kushindwa kupata huduma hiyo.
Sera Ya Ardhi Tanzania
Habari njema ni kwamba serikali ya wilaya ya Arumeru, inatambua jitihada zinazofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Serikali ya wilaya ya Arumeru inakiri mradi huu wa CEDESOTA na mingine katika wilaya hiyo imewasaidia wao kama viongozi kwani muda mwingi walikuwa wakiutumia kusuluhisha migogoro ya ardhi .
“kwa sasa hali imeanza kutengemaa, jamii imeanza kubadilika baada ya kutambua umiliki wa mali ikiwemo ardhi ni haki ya mwanamke na mwanaume, pia wamefahamu kwamba mmiliki mkuu wa ardhi ni serikali”anasema Veronica Patrick Mafulu, ambaye ni afisa ardhi Halmashauri ya wilaya ya Meru.