Wachoma mahindi na wauza Mbogamboga katika Eneo la Feli Kata ya Magole Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro wakisaini Kitabu Cha Rambirambi ikiwa ni ishara ya kuungana na Watanzania wengine kufanya maziko ya Hayati Dkt John Pombe Magufuli.
Wachoma mahindi na wauza Mbogamboga katika Eneo la Feli Kata ya Magole Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro wakiwa katika Maombi maarumu ya kumuombea Hayati Dkt John Pombe Magufuli.
********************************
NA FARIDA SAIDY,MOROGORO
Wachoma mahindi, wauza mboga, matunda pamoja na mamalishe katika eneo la Feli Kata ya Magole Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wamesitisha kwa saa kadhaa shughuli za Biashara zao ili kuungana na Watanzania wote kushiriki mazishi ya Hayati Dokta John Pombe Magufuli wakikumbuka alivyo wajengea vibanda vya kufanyia biashara katika eneo la feli.
Fullshangwe Blog imefika katika eneo hilo la Feli na kushuhudia shughuli za Biashara zikiwa zimesimama huku wafanyabiashara hao wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya kufanya maombi maalumu ikiwa ni ishara ya kushiriki maziko ya mpendwa wao Dokta John Pombe Magufuli.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wajasiliamali hao wamesema wanamkumbuka Hayati Dokta Magufuli kwa vitu vingi hususani kwa kuwa na maamuzi magumu katika kuwasaidia wananchi wa hali ya kama alivyofanyia wao katika Kata ya Magole kwa kuwajengea vibanda vya kufanyia biashara eneo la Feli katika Barabara kuu ya Dodoma.
Aidha Wafanyabiashara hao wamesema wataendelea kuchapa kazi ili kumuenzi huku wakimuomba Rais Mama Samia Suluhu Hasan kufuata nyendo za Hayati Dokta Magufuli.
Hata hivyo Katika viunga mbalimbali vya mji wa Morogoro Wananchi walifuatilia moja kwa moja mazishi ya Hayati Dokta John Pombe Magufuli kupitia Luninga pamoja na mitandao ya kijamii ikiwa ni moja ya njia ya kumuaga Jemedari huyo.