Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Albinus Mgonya (Mwenye suti nyeusi) akiwa ameambatana na ujumbe wake wakiwasili Chuo Kikuu Mzumbe.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Ganka Nyamsogoro, akiweka picha na kitabu cha maombolezo sehemu iliyoandaliwa baada ya kupokea msafara wa Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Mvomero.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe.Albinus Mgonya, (kushoto) akikabidhi kitabu cha maombolezo cha Wilaya ya Mvomero kwa Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Ganka Nyamsogoro
Baadhi ya Wafanyakazi na Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, wakisaini kitabu cha maombolezo
Baadhi ya Wanafunzi wakiwa katika foleni ya kusubiri kusaini kitabu cha maombolezo
****************************************************
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe.Albinus Mgonya, leo Machi 24 amekabidhi kitabu cha maombolezo ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt.John Joseph Pombe Magufuli kwa Uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe, baada ya Wilaya kuzindua kitabu cha maombolezo kiwilaya Jumanne tarehe 23 Machi 2021.
Akikabidhi kitabu cha maombolezo Mhe.Mgonya amesema kuwa kitabu hicho kitazunguka katika Taasisi zote zilizopo wilaya ya Mvomero kwa kipindi cha siku 21 za maombolezo, na kwamba Chuo Kikuu Mzumbe ndiyo taasisi inayozindua utaratibu huo ambapo kitabu hicho kitakaa chuoni hapo kwa muda wa siku tatu mfululizo.
Mhe.Mgonya amesema Hayati Dkt.John Pombe Magufuli alikuwa ni Kiongozi Mzalendo, Mchapakazi, Mwadilifu na aliyependa sana nchi yake na kwamba watanzania wote tunao wajibu wa kuyaenzi na kuyatekeleza mema yote aliyotuachia.
Akipokea kitabu hicho Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof.Ganka Nyamsogoro amesema Chuo Kikuu Mzumbe kimepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa Hayati Dkt. Magufuli na kueleza katika muda mfupi aliohudumu alifanya uwekezaji mkubwa katika miradi ya maendeleo ikiwemo Sekta ya elimu, na kwamba Chuo kikuu Mzumbe ni miongoni mwa Taasisi zilizonufaika na uwekezaji huo ukiwemo uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa mabweni na majengo ya madarasa.
Prof Nyamsogo aliongeza kuwa Chuo kimepokea kwa heshima kubwa kitabu hicho cha maombolezo cha Wilaya na kwamba Wanajumuiya wa Chuo Kikuu Mzumbe watazitumia vyema siku tatu za kusaini kitabu hicho, kwani wanautambua vyema mchango mkubwa uliotolewa na Hayati Dkt.Magufuli.