*************************************************
NA SULEIMAN MSUYA SONGEA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dk.Damas Ndumbaro amesema serikali inaendelea kuhamasisha miradi ya kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu kwa kuwa ina mchango mkubwa kwenye ukuaji wa pato la taifa.
Dk.Ndumbaro amesema hayo wakati wa uzinduzi wa mashine ya kuchakata mazao ya misitu iliyotolewa Shirika la Mpingo na Maendeleo (MCDI), chini ya ufadhili wa Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC).
Program ya FORVAC inatekelezwa chini ya Idara ya Nyuki na Misitu na kufafhiliwa na Serikali ya Tanzania na Finland.
Amesema kinachofanywa na FORVAC na MCDI ni sehemu utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ibara ya 69 kigungu F ambayo inasema kuwepo mashine za kuongeza thamani mazao ya misitu ili kuleta ajira na kusaidia wananchi.
“Misitu ni sekta muhimu sana katika nchi kimazingira, kiuchumi, ajira na ukuaji wa viwanda. Leo tumezindua mashine hii inayochakata tani 5,000 kwa mwaka, mbao 400 kwa siku ni kiwanda kabisa ambacho kinaongeza ajira, kodi na pato la taifa kwa ujumla.,” amesema.
Amesema misitu nchini Tanzania inachukua asilimia 54 ya eneo lote hivyo ikitumiwa kwa matumizi bora itabadilisha maisha ya wananchi.
Dk.Ndumbaro amesema ili sekta hiyo kuendelea kuongoza katika uchangiaji wa pato la taifa ni vema wadau wote kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha taratibu zinafuatwa kwenye kila hatua muhimu kama FORVAC na MCDI wanafanya.
Amesema kwa sasa sekta hiyo inachangia pato la taifa kwa asilimia 21 ambapo Utalii inachangia asilimia 17.5 na misitu asilimia 3.5 hivyo dhana ya mnyororo wa mazao ya misitu itumike kuongeza mchango zaidi.
Waziri Ndumbaro amesema miti na misitu ikivunwa kwa mfumo endelevu itachochea maendeleo hivyo rai yake ni kuona kila wilaya yenye miti inayoweza kuvunwa kiundelevu ikawa na mashine ya kisasa ya kuchakat mazao ya misitu.
Amesema Serikali itahakikisha kila mahali kwenye fursa za misitu inatumiwa kuchochea maendeleo na huduma za kijamii na kuvitaka vijiji kununua mashine za kuchakata.
Waziri amesema wao kama wizara hawatalala kuhakikisha mchango wao kwa pato la taifa unaongezeka.
“Niwaombe wadau wote sekta ya misitu tafuteni Sera ya Misitu ya 1998 na Sheria ya Misitu ya 2002 kuhakikisha lengo la sekta hii kuchangia pato la taifa inatimia bila kuathiri mazingira na maliasili zingine” amesema.
Kwa upande wake Mratibu wa FORVAC Kitaifa, Emmanuel Msoffe amesema wamesukumwa kutoa fedha za ununuzi wa mashine hiyo ili usimamizi wa misitu kuwa endelevu huku ukuaji wa uchumi ukiwepo.
Amesema mashine hiyo ambayo imegharimu zaidi ya shilingi milioni 100 itatumika katika vijiji vya Longosi, Lipagalo Liweta, Litoa, Litumbati vya wilaya ya Songea na vijiji vitano vya wilaya ya namtumbo.
Amesema program hiyo imekuwa na mafanikio kwa kiwango kikubwa katika hatua zote ila kuna changamoto ya masoko na kuahidi kuziifanyia kazi.
Mkurugenzi Mkuu wa MCDI, Makala Gasper amesema wamekuwa wakijishughulisha na uhifadhi wa misitu kwa kushirikiana na Serikali katika kila ngazi jambo ambalo linachangia mafanikio.
Amesema mashine hizo zina mchango mkubwa kwenye kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu ambapo hadi sasa vijiji 61 vimenufaika na kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 2 zinazotumika kwa miradi yaayaaendeleo.
“Tupo katika vijiji 61 wilaya 9 na mikoa 4 ambapo kuna mabadiliko makubwa katika kukuza kipato cha wanavijiji, kuboresha na kujenga huduma za jamii, ajira kupatikana na manufaa mengine mengi,” amesema.
Anasema maratajio yao ni kuhakikisha jamii inayojihusisha na Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) inanufaika pamoja na Serikali.