Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga akifafanua jambo alipotembelea kukagua ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mkoani Rukwa hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga (katikati) akikagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Veta mkoani Rukwa. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Veta wa wizara hiyo, Margaret Mussai na Msimamaizi Mkuu wa Ujenzi wa chuo hicho, Jeremiah Longido.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga amesema Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) cha mkoa wa Rukwa.
Amesema utekelezaji wa mradi huo kwa awamu ya kwanza ulifadhiliwa kwa mkopo kutoka benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na kujengwa na Mkandarasi ambapo mradi ulifikia asilimia 52.
Mhe Kipanga ameeleza kuwa kwa sasa ujenzi utakamilishwa kwa fedha za Serikali kwa kutumia utaratibu wa force akaunti na unatarajia kukamilika ili kuwezesha kuanza udahili Mwezi Julai 2021.
“Napenda kuwatoa wasiwasi wana Rukwa kwani Serikali sasa imetenga Shilingi bilioni 2.5 za kukamilisha ujenzi wa chuo hiki na kwamba tunatarajia ndani ya muda mfupi fedha hizi zitalipwa ili ujenzi uweze kukamilika ifikapo Julai, 2020,” amesema Kipanga.
Awali, akitoa taarifa ya mradi huo, Msimamizi Mkuu wa mradi, Jeremiah Longido amesema awamu ya kwanza ya ujenzi ilianza mwaka 2018 na mpaka sasa umefikia asilimia 52 ambapo umegharimu jumla ya Shilingi bilioni 3.6.
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Carolius Misungwi ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya kumaliza ujenzi wa chuo hicho na kuahidi ofisi yake kutoa ushirikiano katika kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.