Na Dotto Mwaibale, Singida
WABUNGE wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamepata kikombe cha dawa ya Corona yenye uwezo wa kukinga na kutibu ugonjwa wa virusi vya corona iitwayo Shekilindi BOSN. A. iliyotengenezwa na Mbunge wa Jimbo la Lushoto, Shabaan Shekilindi wa Mkoa wa Tanga.
Katika hatua nyingine kwa mapenzi dhidi ya wananchi na watumishi wa umma wa Mkoa wa Singida, Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ambaye ni Mwenyekiti wa wabunge wote wa mkoa huo amemkabidhi dawa hiyo mkuu wa mkoa Dkt.Rehema Nchimbi ili waitumie kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
Mtaturu akimkabidhi dawa hiyo Dkt.Nchimbi baada ya kumalizika kwa kikao maalumu cha ushauri cha mkoa (RCC) kilicho keti mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kuomba kuidhinishiwa bajeti ya Sh. Bilioni 222,188,872,239 ya mwaka wa fedha 2021/2022 ambayo ni zaidi ya bajeti ya Sh. Bilioni 175,619,858, 500 iliyotengwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 alisema dawa hiyo imewasaidia wabunge kwa kiasi kikubwa kujikinga na maambukizi ya Covid 19.
“Mheshimiwa mkuu wa mkoa hivi sasa tupo katika mapambano ya ugonjwa wa Covid 19 ambapo tunatakiwa tuchukue tahadhari zote za kujikinga nao kama tulivyo sisitizwa na Rais wetu Dkt.John Magufuli na wataalamu wa afya,” alisema Mtaturu.
Alisema baada ya Mbunge mwenzao huyo kuitengeneza dawa hiyo walipata kikombe kama kile alichokuwa akikitoa Babu wa Loliondo Ambilikile Mwasapile.
” Kusema kweli kikombe cha dawa hiyo kimetusaidia sana ndio maana hamjasikia wabunge tukisumbuliwa na changamoto hiyo. Mheshimiwa mkuu wa mkoa nakukabidhi dawa hii ambayo kichupa kimoja kinauzwa sh.30,000 nawe uone namna ya kufanya utaratibu kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wetu na watumishi wa umma mkoani hapa.” alisema Mtaturu.
Alisema watawasiliana na mtengenezaji wa dawa hiyo kuona namna ya kuisafirisha hadi Singida kwa ajili ya wale watakao ihitaji kwani suala la afya ni la muhimu kwa kila mmoja wetu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mtaturu alisema dawa hiyo imeonekana inafaa kwa matumizi na inauwezo wa kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo baada ya kuidhinishwa na vyombo husika vya Serikali ikiwemo Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania (NIMR) na kukabidhiwa vyeti vya udhibitisho.