*******************************
Kampuni ya huduma za mafuta Jijini Mwanza ya Petro Africa imekabidhi msaada wa mifuko 200 ya Saruji kuunga mkono jitihada za mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula katika kuboresha sekta ya elimu ndani ya jimbo hilo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mwakilishi wa kampuni ya Petro Africa Bwana Ahmeid Mohameid Ally amesema kuwa wamefikia uamuzi wa kuchangia saruji hiyo kwaajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya elimu ikiwemo madarasa, vyoo na ofisi katika shule za jimbo la Ilemela baada ya kupokea ombi la mbunge wa jimbo hilo sambamba na jitihada zake katika kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo kupitia Sera yake ya utatu ambapo wananchi wanahimizwa kuanzisha misingi, mbunge anatoa tofali zote za ujenzi wa mradi husika na kisha mkurugenzi wa manispaa anakamilisha mradi huo
‘.. Mama huyu anapambana sana katika kuimarisha sekta ya elimu ndani ya jimbo lake, Nasi tukaona tutoe kidogo tulichonacho ili kumtia nguvu katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa shule za Ilemela ..’ Alisema
Aidha Bwana Ahmeid akaongeza kuwa wataendelea kushirikiana na mbunge huyo katika kuwaletea wananchi maendeleo sanjari na kuomba wadau wengine kujitokeza na kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli ikiwemo sera na mpango wake wa kutoa elimu bila malipo.
Kwa upande wake, Katibu wa Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ilemela Bwana Kazungu Safari Idebe mbali na kuishukuru kampuni hiyo kwa msaada ilioutoa akaongeza kuwa Mbunge kupitia fedha za mfuko wa jimbo mapema mwezi Machi mwaka huu alitoa mifuko 2000 ya saruji kwa manispaa ya Ilemela kwaajili ya ufatuaji wa tofali zitakazotumika katika ujenzi wa miundombinu ya elimu, afya na mingine ikiwemo ujenzi wa ofisi za serikali za mitaa, Hivyo kuja kwa msaada huo kutaongeza kasi ya ukamilishaji wake
Zoezi la makabidhiano ya mifuko hiyo ya saruji lilishuhudiwa pia na mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Dkt Mathias Severine Lalika na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela ambae pia ni afisa ardhi na mipango miji Ndugu Shukrani Kyandi.