Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dk.Severine Lalika (kulia) akipokea moja ya mifuko 184 ya vifaa vya wajawazito kutoka kwa Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation (TD & CF), Alhaji Sibtain Meghjee juzi, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa wilayania Ilemela.
Mifuko yenye vifaa hivyo vilivyogharimu sh.5,550,000 kama inavyoonekana.
Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation (TD & CF),Tawi la Tanzania, Alhaji Sibtain Meghjee (kushoto), akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dk.Severine Lalika kuhusu baiskeli mbili za walemavu kabla ya kumkabidhi juzi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.Basikeli hizo za kisasa zimegharimu sh. milioni 1.2.
Gari la taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TD & CF) lenye namba T 989 CHV likiwa limebeba vifaa mbalimbali vilivyotolewa bure na taasisi hiyo ili kuwasaidia akina mama wajawazito wakati wa kujifungua.
……………………………………………………………………………………………….
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
SERIKALI imesema kuwa inathamini misaada ya kijamii inayotolewa na The Desk & Chair Foundation (TD & CF),katika kuunga mkono juhudi za kuwahudumia wananchi wakiwemo wnye mahitaji maalum.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dk. Severine Lalika alisema juzi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, kwenye Maadhismisho ya Siku ya Wanawake Duniani,wakati akipokea msaada wa vifaa vya kujifungulia akinamama na baiskeli za walemavu.
Alisema serikali kwa namna ya pekee inaishukuru TD & CF kwa kuunga mkono juhudi zake za kuhakikisha Watanzania wenye mahitaji maalum nao wananufaika na wanajisikia faraja kwa kupata huduma za kijamii kama hizo.
“Nikuhakikishie kwa misaada mnayotoa kama ujenzi wa vyoo kwa shule zetu za msingi na baadhi ya shule za sekondari,serikali tunaithamini sana misaada ya namna hiyo,”alisema Dk. Lalika.
Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, Tawi la Tanzania, Alhaji Sibtain Meghjee,alisema msaada huo wa vifaa mifuko 184 kwa ajili ya akinamama wakati wa kujifungua na baiskeli mbili za watu wenye ulemavu umegharimu sh.milioni 6.7.
Alisema walifanya utafiti wao wakabaini akina mama wajawazito wana changamoto ya kukosa vifaa wanapokwenda kujifungua na baada ya kuguswa na changamoto hiyo mwaka huu kwenye madhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani wameamua kutoa mifuko 184 yenye thamani ya sh.milioni 5.55 vigawiwe bure ambapo mwaka jana waligawa mifuko 280.
Pia baiskeli mbili kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye walemavu zenye thamani ya sh.milioni 1.2 na kufanya idadi ya vyenzo hizo zilizotolewa bure kwa watu hao wenye mahitaji maalum kufikia jumla ya baiskeli 569.
Alhaji Meghjee alisema taasisi hiyo yenye makao makuu nchini Uingereza ilianzishwa mwaka 2003 na Watanzania wenye asili ya Kiasia (wote wazaliwa wa Mwanza) na kwa Tanzania ilisajiliwa na kuanza kazi mwaka 2004.
“Taasisi hii tulianzisha mwaka 2003 ili kusaidia jamii na waalinzishi wote ni wazaliwa wa hapa Mwanza na tunafanya kazi bila kubagua kwa kusaidia jamii katika sekta za afya, elimu na maji,”alisema
Aidha alhaji Meghjee alieleza kuwa taasisi hiyo inajishughulisha na utoaji wa misaada ya kijamii ikigharamia baadhi ya matibabu ya wagonjwa,ujenzi wa vyoo,madarasa,sare za shule na utengenezaji wa madawati.