Kisima cha maji kinachohudumia vijiji viwili vya Chiwanda na Umoja katika kata ya Chiwana wilayani Tunduru mkoani Ruvuma ikiwa ni miongoni mwa miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa na wakala wa maji vijijini Ruwasa wilayani Tunduru.
moja kati ya tenki la kuhifadhia maji linalohudumia wananchi wa kijiji cha Chiwana na Umoja kata ya Chiwana wilaya ya Tunduru lililojengwa na wakala wa usambazaji maji vijijini Ruwasa wilayani humo.
Picha zote na Muhidin Amri,
…………………………………………………………………………………………………
Na Muhidin Aamri,Tunduru
WANANCHI na viongozi wa serikali za vijiji na kata wilayani Tunduru, wamekumbushwa wajibu wao kuhakikisha wanasimamia miradi na kuwa walinzi wa miundombinu ya maji inayotekelezwa, yenye lengo la kuchochea maendeleo katika maeneo yao na kuboresha maisha yao.
Kauli hiyo imetolewa jana na kaimu Meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini Ruwasa wilaya ya Tunduru Emmanuel Mfyoyi, wakati akikugua mradi wa maji kijiji cha Chiwana kata ya Chiwani wilayani humo.
Mradi wa maji Chiwana unatekelezwa na Ruwasa kwa gharama ya shilingi milioni 175 umelenga kuwaondolea kero ya maji safi na salama wananchi wapatao 5,6000 wa kijiji cha Chiwana na Umoja wenye vituo 8 vya kuchotea maji ambapo ujenzi wake hadi sasa umekamilika kwa asilimia 98 na wananchi wameanza kupata huduma ya maji.
Mfyoyi alisema,miradi yote ya maji inayoendelea kutekelezwa na Serikali ina lenga kumaliza changamoto ya maji na kuwaondolea usumbufu wananchi kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kutafuta maji.
Alisema, miradi hiyo italeta tija iwapo wananchi na jamii mzima wataitunza na kuitumia kwenye shughuli za kiuchumi na watendaji wa serikali kutekeleza wajibu wao kwa kulinda na kuisimamia, badala ya kuichia Ruwasa ndiyo kuwa mlinzi wa miradi husika .
Katika wilaya ya Tunduru yenye zaidi ya wakazi 256,510 wananchi wanaopata maji kwa sasa ni 164,166 sawa na asilimia 64 na lengo la Ruwasa kuhakikisha hadi kufikiwa mwishoni mwa mwaka huu idadi ya watu wanaopata maji safi na salama inaongezeka kutoka asilimia 64 ya sasa.
Katibu wa jumuiya wa watumia maji wa vijiji hivyo Said Mawimba alisema,kabla ya mradi huo wananchi wa vijiji vya Chiwana na Umoja walilazimika kupata maji kutoka kwenye visima visivyo rasmi na wengine kwenye mito inayopita katika maeneo yao.
Hata hivyo,kukamilika kwa mradi huo kumeleta nafuu kubwa kwa wananchi ambao wameanza kunufaika na kutumia maji ya bomba kwenye shughuli zao za kila siku na kuondokana kupata ugonjwa wa matumbo na kipindu pindu.
Alisema, wakati mwingine wananchi wanapokwenda mtoni kuchota maji wanakutana na changamoto mbalimbali na wapo waliowahi kupoteza maisha kwa kuliwa na wanyama wakali kama Simba pindi wanapokwenda kutafuta maji mbali na makazi yao.
Wananchi wa kijiji hicho,wameshukuru kufikishiwa huduma ya maji safi na salama kwani imemaliza kero waliyonayo kwa muda mrefu ambayo ilichangia kusua sua kwa shughuli za maendeleo.
Sikuzan Kassim mkazi wa Chiwana alisema, kabla Ruwasa kupeleka huduma ya maji katika kijiji chao walilazimika kuamka usiku wa manane kwenda kutafuta maji mbali na makazi yao.
Alisema, hali hiyo ilikuwa kero kubwa sio kutokana na kukosekana kwa huduma ya maji karibu na makazi yao tu bali ilisababisha baadhi ya ndoa kuvunjika kwa kile walichoeleza wanawake kuchelewa kurudi nyumbani.