Mbunge wa viti maalum Ritta Kabati akiwa katika matukio tofauti wakati alipokuwa mgeni rasmi wa siku ya mwanamke Mwamba ulivyofanyika mjini dodoma
………………………………………………………………………………………
MBUNGE wa viti maalum mkoa wa Iringa Dkt. Ritta Kabati amewataka wanawake kuwa msingi wa mapato katika familia zao na Taifa kwa Ujumla.
Dkt. Kabati ameyasema hayo alipokualikwa katika kituo cha redio C Fm iliyopo Jijini Dodoma katika hafla ya utoaji wa tuzo za wanawake waliofanya vizuri katika mambo mbalimbali kwa mwaka 2020.
“Wanawake wawe chanzo cha mapato nyumbani wawe ndiyo msingi wa Mapato Katika familia zao, hii itasaidia hata kuleta usawa pamoja na heshima katika familia”
Kabati amesema yeye kama kiongozi tayari ameanzisha mkakati wa kumnyanyua Mwanamke wa Iringa kiuchumi kwa kuanzisha vikundi na na kuvipa mafunzo ya Kilimo na ufugaji.
“Kwa sasa nimeanzisha mkakati maalum wa kuwanyanyua wanawake kiuchumi kwa kuwahamasisha waunde vikundi na kuvipatia mafunzo ya kilimo na ufugaji. Mambo yakikaa sawa wanawake wa Iringa tutazalisha sana mazao ya biashara” Alisema
Aidha ameongeza kwa sasa wanawake ni lazima wawe na uthubutu katika kuwania nyazifa mbalimbali ili kuongeza usawa wa kinjisia.
“Wanawake hususani vijana msiogope kuingia katika uongozi mkiona nafasi hizo jitokezeni hii ndiyo njia pekee ya kuleta usawa katika jamii. Hakuna matatizo ya Wanawake yatakayotatuliwa vizuri na Wanaume bali wanawake wenyewe.”
Amesema kuwa ili kuwa na viongozi wengi wa kike katika taasisi binafsi na za serikali ni vyema wanawake wakaacha uoga na badala yake waweze kujitokeza na kuonesha uwezo wao pindi wanapopata nafasi mbalimbali za uongozi katika jamii.
“ili tuweze kuwa wengi ni vyema tujitokeze kuwania nafasi za uongozi na pia tuoneshe uwezo wetu wote ili kuhakikisha tunaaminika na pia tunawahamasisha zaidi wanawake wengine kuwania nafasi hizo”
Kuhusu kauli mbiu ya siku ya wanawake ya “Wanawake katika uongozi, chachu kufikia Dunia yenye usawa” Dkt Kabati amesema kuwa kauli hiyo inatekelezeka kwa wanawake kuamua kuwatumikia wananchi wao kwa uadilifu.
“Kauli mbiu ya safari hii inatekelezeka, inatekelezeka kama wanawake wataamua kufanya kazi kwa uadilifu na uzalendo kwa Taifa letu.”
Akizungumza kwa niaba ya Wafanyakazi wa C FM redio, Veronica Komba amempongeza Mbunge Kabati kwa kuwa mwanamke Mwamba kutoka mkoa wa Iringa kutokana na kazi nyingi na misaada anayotoa katika jamii anayoiongoza.
“wewe ni Mwanamke Mwamba, kwa sababu unajitoa sana katika jamii, unafanya kazi zinazoigusa jamii yako na huu ndio Umwamba tunaousemea sisi Kama C FM Dodoma”
Aidha, Bi. Komba amewashauri wanawake hususani wafanya biashara kutumia vyombo vya habari katika kufanya matangazo ya biashara zao ili kuongeza fursa ya kuwa na masoko katika maeneo mengi.