Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo prof. Elisante Ole Gabriel akimsaidia mwananchi kuchota maji kutoka kwenye kisima kwa ajili ya kunyweshea mifugo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo prof. Elisante Ole akikagua Mto Kou katika Kijiji cha Magara ambao wafugaji wamekatazwa kunyeshwea mifugo ili kulinda mazingira.
***************
Na. Edward Kondela
Serikali imesema inatafuta suluhu ya kudumu ya upatikanaji wa maji kwa mifugo iliyopo katika kata za Nkaiti, Mwada na Magara zilizopo Wilaya ya Babati Mkoani Manyara bila kuathiri mazingira ya Mto Kou unaopita katika kata hizo.
Akizungumza na baadhi ya wananchi katika Kata ya Mwada mara baada ya kutembelea vijiji vya Vilima Vitatu na Magara ili kutafuta suluhu ya wafugaji kupata maji na malisho ya mifugo yao bila kuathiri Mto Kou uliopo katika Hifadhi ya Burunge ambao ni chanzo cha Ziwa Manyara, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuna haja ya kutafuta njia ya kutatua baadhi ya mambo ili kupata suluhu ya matatizo hayo.
“La kwanza kabisa ni upatikanaji wa maji tuangalie namna ya upatikanaji wa maji haraka, la pili tutaunda timu ya wataalam kutoka Wizara za Mifugo na Uvuvi, Maliasili na Utalii, Ardhi, TAMISEMI, Maji na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali, la tatu kuna haja ya kuona hawa watu ambao wameondolewa wanatakiwa kwenda wapi na watakwendaje, pia ni vyema kuendelea kushirikiana serikali na wadau hautakaa ufanikiwe kwa kushindana na serikali kikubwa ni mazungumzo na kushauriana pia ule mpango wa matumizi bora ya ardhi unapaswa pia kuangaliwa vizuri.” Amesema Prof. Gabriel
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Babati Bibi Elizabeth Kitundu akizungumza na wafugaji wanaoishi katika eneo la malisho katika Kijiji cha Vilima Vitatu, amewataka waondoke na kwenda kuishi eneo lingine jirani na hapo la Mfulang’ombe ili kupisha eneo hilo libaki kwa malisho ya mifugo pekee.
“Hapa bado serikali ya wilaya na mkoa inasema kwamba hamstahili kukaa hapa eneo lenu linaeleweka mnalotakiwa kukaa ni Mfulang’ombe mtakuwa mnatoa ng’ombe kule mnakuja kuchungia hapa ili muendelee sasa kushirikiana na serikali kuweka miundombinu ya kutosha na maji na hapa mtakuwa mnachungia kwa hiyo muisikilize serikali inavyosema kama kutakuwa na maelekezo mengine mtajulishwa.” Amesema Bibi Kitundu
Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa vijiji vilivyopo katika vijiji ambavyo Mto Kou unapita wamesema ni vyema wakapata maji ya kutosha kwa ajili ya mifugo yao bila kuathiri mazingira ya mto ambapo baadhi ya vijiji vimeamua kuchimba visima ili kupata maji ya mifugo yao.
Mara baada ya kikao cha Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo na Prof. Elisante Ole Gabriel wananchi katika Kata ya Mwada, alikaa na viongozi wa Mkoa wa Manyara, Wilaya ya Babati, viongozi wa vijiji na wafugaji ambapo wamejadili baadhi ya mambo ili kupata suluhu ya maji na malisho kwa ajili ya wafugaji wanaoishi katika kata za Nkaiti, Mwada na Magara.