…………………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Mtwara
Katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 8, Waandishi wa habari Wanawake kupitia chama cha wanahabari Mkoani Mtwara wametumia siku hiyo kuwatembele wanafunzi wa kike wanaosoma shule ya Mtwara Sisters Seminary iliyopo Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Lengo la wanahabari hao kutoka vyombo mbalimbali vya habari kuandaa ziara hiyo limekuwa ni kukutana na vijana wa kike wanaosoma shuleni hapo, kuzungumza nao, kuwati moyo, kuwafariji na kuwapa stadi za maisha wawapo shuleni na hata majumbani mwao.
Sambamba na hilo, wanahabari hao pia wametoa msaada wa taulo za kike kwa wanafunzi ili kuendelea kuwapa tabasamu wakati wote wanapokuwa masomoni.
Waratibu wa tukio hilo Bi. Grace Kasembe na Bi. Mwajuma Kitwana, kwa nyakati tofauti wametoa sababu za kuamua kutumia siku ya wanawake duniani kukutana na vijana hao wa Mtwara sisters Seminary wakisema kuwa ni uamuzi ambao umezingatia afya za wanafunzi wa kike wanapokuwa katika siku za hedhi.
Bi. Grace Kasembe ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Mtwara, amesema wameona vyema kushiriki siku hii muhimu na wanafunzi hao ili kuwatia Moyo katika msomo pia ili kuwajenga kisaikolojia maana ni viongozi wajao.
Ameeleza kuwa wamekuwa na utaratibu wa kushiriki matukio mbalimbali kwa kuifikia jamii kwa namna tofauti, hivyo tukio la leo halitakuwa la mwisho.
Kwa upande wake Bi Mwajuma Kitwana ambaye ni mratibu wa tukio hilo amewashukuru wadau walioshirikiana nao katika kuadhimisha siku hii, huku akiwaa wanafunzi hao kuthamini pesa inayotolewa na wazazi wao na kuwekeza kwenye elimu wanayoipata maana ndio msingi wa maisha.
Muwakilishi wa wadau walioshiriki kuwezesha tukio hilo ambaye ni meneja wa Shirika la Bima la Zanzibar Bw. Bahatisha Suleiman amesema ushiriki wao katika siku ya wanawake duniani umetokana mahusiano mazuri ya kitaasisi yaliyopo na wanahabari kupitia chama cha waandishi wa habari mkoa wa Mtwara.
Ameeleza kuwa juhudi zinazofanya na MTPC za kuwaunganisha wadau pamoja na waandishi wa habari, zimeongeza mahusiano mema na kuwafanya wadau kuhamasika zaidi kuungana na waandishi wa habari katika masuala mbalimba huku akiahidi kuwa wataendeleza ushirikiano huo kwa waandishi wa habari kupitia chama chao cha wanahabari mkoa wa Mtwara.
Amewakumbusha wanafunzi wa Mtwara Sisters Seminary kuzingatia elimu na kufuata maadili kuhusu yale wanayofundishwa na waalimu, huku akisisitiza kwamba utaratibu huo uliotumiwa na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, unapaswa kuigwa na taasisi zingine.
Wadau walioshirikiana na wanahabari katika kufanikisha zoezi hilo kupitia Mtwara Press Club ni Benki ya watu wa Zanzibar – PBZ, Shirika la Bima la Zanzibar – ZIC, Mamlaka ya Mapato Tanzania – TRA, Tanzania Breweries – TBL, Ndanda Splash na BOTNET Computers.
Maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yaandhimishwa Kimkoa mkoani Mtwara ambapo kauli mbiu ni “wanawake katika uongozi, CHACHU KUFIKIA DUNIA yenye USAWA”