Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Missaile Mussa akizungumza kwenye kikao cha ushauri cha Mkoa huo ambapo mpango wa bajeti ya sh198 bilioni ilipitishwa na wajumbe, katikati ni Mkuu wa Mkoa huo Joseph Joseph Mkirikiti na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul.
Mbunge wa viti maalumu Regina Ndege akizungumza kwenye kikao cha ushauri cha Mkoa huo kilichokutana mjini Babati na kupitisha mpango wa bajeti ya sh198 bilioni.
…………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Babati
MKOA wa Manyara na Halmashauri zake saba za wilaya, umependekeza mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 kwa kutumia kiasi cha sh198 bilioni.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Missaile Mussa ameyasema hayo mjini Babati juzi kwenye kikao cha kamati ya ushauri cha mkoa huo.
Mussa amesema kati ya fedha hizo ruzuku kutoka serikali kuu ni sh181.9 bilioni na mapato ya ndani ni sh16.1 bilioni, sh129.4 bilioni ni mishahara, matumizi ya maendeleo ni sh42.6 bilioni na matumizi mengine ni sh9.8 bilioni.
Amesema ruzuku kutoka serikali kuu kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni sh42.6 bilioni, kati ya fedha hizo sh23.1 bilioni ni fedha za ndani na sh19.5 ni fedha za nje.
Amesema mapato ya ndani ya mamlaka ya serikali za mitaa ni sh16.1 bilioni, kati ya fedha hizo sh13 bilioni ni mapato ya vyanzo visivyolindwa na sh3 bilioni ni kutoka vyanzo lindwa.
“Kiasi cha sh5.2 bilioni kutoka vyanzo visivyolindwa kitaelekezwa katika shughuli za maendeleo, sh6.5 bilioni kwenye matumizi mengine na sh1.3 kitaelekezwa katika mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu,” amesema.
Hata hivyo, amesema vipaumbele vya mkoa huo ni kilimo, uanzishwaji wa viwanda vidogo na vya kati vya kuchakata mazao ya kilimo, ufugaji, uchimbaji madini na kuongeza mapato ya ndani.
Amesema wamelenga kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuimarisha ufuatiliaji na tathimini na ugatuaji wa madaraka.
Mbunge wa viti maalum wa mkoa wa Manyara, Regina Ndege amesema halmashauri zinapaswa kutekeleza utoaji wa mikopo kwa makundi maalumu.
Ndege amesema makundi maalumu ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanatakiwa kupatiwa kwa wakati mikopo kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani.