Pichani ni Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa nchini Dkt Noel Lwoga
Wafanyakazi Wanawake wa Makumbusho ya Taifa kutoka Makao Makuu, Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni pamoja na Wakijiji cha Makumbusho Dar es Salaam, wakiwa viwanja vya Mlimani City kuungana na wanawake wengine kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani.
Kulia ni Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu Bi Nuru Sovellah, na kushoto ni Mkuu wa kitengo cha Mipango Bi Neema Mbise (Wote wa Makumbusho ya Taifa) wakiwa na bango la Taasisi hiyo katika viwanja vya Mlimani City kuungana na wanawake wengine kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani.
*****************************************
Na Sixmund Begashe
Watanzania washauriwa kuenzi mchango wa wanawake katika jamii kwa kuwa wamekuwa chachu kubwa katika mapambano ya ukombozi, uchumi, malezi, ubunifu, kama hitoria ya nchi inavyo dhihirisha dhahiri kabla ya ukolono, kipindi cha Ukoloni hadi kupata Uhuru na katika maisha ya leo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga kwa lengo la kuwapongeza Wanawake ambao ni wafanyakazi wa Taasisi hiyo ya Kitafiti na elimu kwa kuungana na wanawake wote Duniani kusherekea siku ya Wanawake kimataifa.
Dkt Lwoga ameongeza kuwa tuendelee kumshukuru Mungu kwa afya njema na fursa ya kusherekea siku hii adhimu Duniani kwani nchi nyingine nyingi zimeshindwa kusherekea kutokana na kufungiwa kutoka nje kwa sababu ya gonjwa linalotikisa ulimwengu la korona.
“Historia inaonesha dhahiri mchango wa Mwanamke katika mapambano ya ukombozi, uchumi, malezi, uhifadhi mazingira na utamaduni na maendeleo kwa ujumla. Wanawake kama walezi, washawishi, wavumilivu, wabunifu na majasiri, ni nguzo kubwa ya ufanisi katika kazi za Makumbusho ya Taifa” Amesema Dkt Lwoga
Wakati wa Sherehe hizi, Dkt Lwoga aliwahasa wafanyakazi hao, kutafakari namna watakavyoliendeleza shirika hilo la Makumbusho, na hasa kutumia fursa na uwezo wa Mwanamke kuboresha utekelezaji wa majukumu hasa kipindi hiki cha mabadiliko ya dhana, dira, uendeshaji na taswira ya Makumbusho ya Taifa.
Akishukuru kwa niaba ya wafanyakazi wanawake wote wa Makumbusho ya Taifa, Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Bi Nuru Sovellah, amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo kwa uchapaji kazi wake usio bagua jinsia wa hali ya mtu na kuhaidi wao kama wanawake wa Taasisi hiyo nyeti katika uhifadhi wa urithi wa asili na Utamaduni kutafanya kazi kizalendo kwa manufaa ya watanzania wote.
Siku ya Wanawake Duniani usherekewa kila mwaka Machi 8, na kwa mwaka huu, Wanawake wa Makimbusho ya Taifa wameungana na wanawake wengine duniani kwa kufanya shughuli mbali mbali (ndani ya wiki) kama vile kuhamasisha jamii kutembelea Makumbusho za Taifa nchini, kuzindua onesho linaloelezea Mchango wa Mwanamke katika ukombozi wa Bara la Afrika na program ya “Twenzetu Makumbusho”.