*************************************
Na Mwandishi wetu, Babati
WAKALA wa barabara (TANROADS) Mkoani Manyara imejipanga kutekeleza matengenezo ya kilomita 1,869.2 za barabara na madaraja 130 kwa makisio ya sh15.3 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.
Meneja wa TANROADS Mkoani Manyara, mhandisi Bashiri Rwesingisa ameyasema hayo mjini Babati kwenye kikao cha bodi ya barabara ya mkoa huo.
Mhandisi Rwesingisa amesema kwa upande wa barabara zinazosimamiwa na TANROADS mkoani Manyara, miradi 20 ya maendeleo ya gharama ya sh4.8 bilioni itatekelezwa.
“Miradi 17 ya ukarabati kwa makisio ya sh3.7 bilioni na miradi sita ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na mradi mmoja wa usanifu ya sh1.1 bilioni,” amesema mhandisi Rwesingisa.
Amesema kazi nyingine ni kuendeleza usimikaji taa za barabarani, ujenzi wa madaraja ya Bisgeta barabara ya Mogitu-Haydom na kukamilisha daraja la Chubi barabara ya Singe-Sukuro.
“Pia kuna madaraja mawili ya barabara ya Mirerani-Landanai, daraja la Sunya barabara ya Kijungu-Sunya-Dongo na ujenzi na ukarabati wa kilomita 9.3 kwa kiwango cha lami,” amesema mhandisi Rwesingisa.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti amewataka viongozi watimize wajibu wao katika suala zima la utunzaji wa barabara.
“Pamoja na hayo tuhakikishe kuwa barabara zinatengenezwa na kutunzwa ili zitumike na hasa wananchi wa hali ya chini wakiwemo wakulima wanaosafirisha mazao yao kutoka shambani,” amesema Mkirikiti.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alisema baadhi ya barabara za pembezoni za mjini Babati zinapaswa kukarabatiwa ili ziweze kupitika kwa muda wote.
Naibu Waziri Gekul alisema pia suala la ujenzi wa uwanja wa ndege wa mkoa huo linapaswa kupewa kipaumbele ili ujenzi wake uanze mara moja.
Mbunge wa Jimbo la Hanang’ mhandisi Samwel Hhayuma amesema ahadi ya kujengwa kwa barabara ya lami Katesh hadi Haydom inapaswa kutekelezwa na pia barabara za michepuko ziingizwe kwenye mpango wa ujenzi.
Mbunge wa Jimbo la Kiteto, wakili msomi Edward Ole Lekaita ameeleza kuwa daraja kwenye kata ya Sunya limesababisha changamoto ya kupitika pindi wananchi wakitaka kuelekea kupata huduma ya matibabu katika kituo cha Sunya na pia barabara zilizopo kwenye ilani kutoka Arusha kwenda Dodoma kupitia Kiteto isitafsiriwe kuwa ni nyingi.
Mbunge wa jimbo la Mbulu mjini, Paul Isaay amesema wakulima wanapata wakati mgumu pindi wakitaka kutoa mazao mashamba kwani vibao vya kuruhusu uzito wa magari ni tani tatu pekee kwenye baadhi ya maeneo.
Mbunge wa jimbo la Mbulu vijijini Flatei Massay amesema maneno ya mchakato, upembuzi yakinifu na usanifu yanapaswa kutekelezwa kwa vitendo ili ujenzi wa barabara ya lami ya Karatu, Mbulu, Haydom, Singida uanze.
Mbunge wa viti maalumu Regina Ndege amesema wanapaswa kushirikiana kati ya wabunge na vitongozi wengine ili kuhakikisha barabara zilizoahidiwa kwenye ilani ya uchaguzi zinatekelezwa.
Mbunge wa Vijana Taifa, Asia Halamga amesema baadhi ya wanaosafisha mazingira ya barabara kwenye wilaya ya Kiteto hawakuwalipa kwa wakati vijana wanaosafisha barabara hivyo ikawalazimu yeye na mbunge wa Jimbo hilo Ole Lekaita wawape fedha hizo.
Mkazi wa Mjini Babati, Anaufoo Ulomi amesema visima vya maji vinapaswa kuchimbwa pembeni ya barabara ili majanga yakitolea maji yapatikane kwa urahisi.