****************************************
Nteghenjwa Hosseah, Kilimanjaro
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Gerald Mweli ametembelea shule ya Sekondari ya Wavulana Umbwe iliyopo Halmashauri ya Moshi Dc Mkoani Kilimanjaro na kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo unaotekelezwa na mradi wa lipa kulingana na matokeo (EP4R) na kusimamiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Akiwa Shuleni hapo Mweli amesema ameridhishwa na ukarabati uliofanyika ambao kwa kiasi kikubwa umebadilisha muonekano wa shule na kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia.
Akitoa taarifa ya ukarabati wa shule hiyo Mkuu wa shule Elirehema Mungaya amesema walipokea shilingi Bilioni 969 toka Serikalini kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo.
“Kutoka katika hela hiyo kazi zilizofanyika
ni ukarabati wa mabweni yote 13, vyoo vyenye matundu 32, mabafu yenye vizimba 40, eneo la kufulia, bwalo la chakula, jiko, madarasa yote 22,jengo la karakana, maabara 3, maktaba 1, vyumba vya Kantini na duka pamoja na mifumo ya maji safi na maji taka” amesema Mwl Mungaya.
Sambamba na kazi hizo Mwl. Mungaya alinainisha kazi za nyongeza walizofanya kutokana wa matumizi mazuri ya fedha kuwa ni kuweka mfumo wa majiko ya Gesi 6 na kuni banifu 2, matenki 6 yenye uwezo wa kuhifadhi maji Lita 60,000, mfumo wa utoaji maji ya mvua, kurekebisha vitanda vyote, makabati ya wanafunzi, njia za kutoka mabwenini na kuongeza viwanja vya michezo.
‘Pamoja na kazi za msingi na za nyongeza zilizofanyika tumetumia jumla ya shili Bil. 792 hivyo tuna salio la shilingi bil 156’ alisema Mkuu wa shule Mwl Mungaya.
Baada ya taarifa hiyo Mweli alisema ameridhishwa na kazi kubwa iliyofanyika na namna ambavyo fedha zimesimamiwa.
“Kutokana na salio mlilobakisha na maombi ya matumizi mliyowasilisha asilimia 50 ya fedha hizo ziende kwenye ukarabati wa nyumba za Walimu kisha Jengo la Utawala halafu mtaendelea na maeneo mengine ya utawala.
Shule ya Sekondari Umbwe (Mti safi huzaa matunda mema) ilianzishwa na shirika la kidini la Holly Ghost Farthers la Kikatoliki mwaka 1949 na baadae ilichukuliwa na Serikali mwaka 1969.
Hivi sasa shule hii ina miaka zaidi ya 70 na haijawahi kukarabatiwa tangu ijengwa lakini kupitia Serikali ya Awamu wa Tano fedha zimepatikana na shule imekarabatiwa kwa ubora wa hali ya juu.