Taswira ya nyumba ya mkazi wa Kijiji cha Kizinga, wilayani Muleba, Venancia Joanes, kama ilivyonaswa muda mfupi kabla ya Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) kuiwashia umeme akiwa katika ziara ya kazi, Julai 17, 2019.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (kulia), na Mbunge wa Muleba Magharibi Charles Mwijage, wakisikiliza kwa makini salamu kutoka kwa viongozi mbalimbali wa Serikali na Vyama vya Siasa, wakati wa hafla ya uwashaji umeme katika kijiji cha Kizinga wilayani Muleba, Julai 17, 2019.
*******************
Na Veronica Simba – Kagera
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amewasha rasmi umeme katika kijiji cha Kizinga, Kata ya Bulyakashaju wilayani Muleba, Mkoa wa Kagera Julai 17, 2019 na kuibua shangwe kwa wananchi wa eneo hilo.
Tukio hilo lilifanyika katika nyumba ya mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Venancia Joanes ambaye alikiri mbele ya Waziri kuwa alilipia shilingi 27,000 tu kama ambavyo Serikali imeagiza kuwa gharama za uunganishwaji umeme vijijini, zisizidi kiasi hicho.
Akizungumza na wananchi wa Kizinga, Waziri Kalemani aliwataka kuiga mfano wa Mama huyo ambaye pamoja na kuwa na nyumba ya tope, ameunganisha umeme.
“Wananchi nawasihi muige mfano wa huyu Mama ili nanyi muunganishiwe umeme katika nyumba zenu. Sisi kama Serikali tulikwishaweka wazi kuwa hatubagui aina ya nyumba kwani wananchi wote wanataka maendeleo,” alisema Waziri.
Katika hatua nyingine, Waziri amekerwa na kukemea utendaji kazi duni wa Mkandarasi aliyekuwa akitekeleza Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II), wilayani Muleba na hivyo akaagiza kufanyika mabadiliko ya wasimamizi mbalimbali wa Mradi huo upande wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Waziri alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga kufanya mabadiliko ya watendaji waliokuwa wakisimamia Mradi huo wilayani Muleba kwa lengo la kuboresha utendaji kazi.
Aidha, aliuagiza Uongozi wa TANESCO kumchukulia hatua za kimkataba Mkandarasi huyo ikiwa ni pamoja na kumkata asilimia 10 ya malipo yake na hata kumfkisha mahakamani ikibidi, kutokana na kutotekeleza Mradi kadri ya makubaliano.
“Zaidi ya Transfoma 110 katika Mkoa huu zimeharibika na hazijafanyiwa matengenezo, Nguzo nyingi zimechimbiwa lakini hazijafungwa nyaya, mashimo mengi yamechimbwa lakini hayajasimikwa nguzo, baadhi ya maeneo hata Transfoma hazijafungwa. Huu ni uzembe wa hali ya juu na hatuwezi kuuvumilia,” alisema Waziri.
Waziri alimtaka Meneja wa TANESCO mkoani Kagera, Mhandisi Francis Maze, kuyafanyia kazi maeneo yote yanayohitaji marekebisho ya miundombinu ya umeme hususan nguzo na transfoma, kabla ya mwisho wa mwezi Agosti mwaka huu ili kuwaondolea kero wananchi.
“Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ametupatia pesa ya kurekebisha miundombinu ya umeme iliyochakaa au kuharibika; na mimi siwezi kupewa pesa halafu nikashindwa kazi. Hivyo nakuagiza Meneja kufikia mwezi wa Nane mwishoni uwe umekamilisha kazi hiyo.”
Pia, Waziri aliuagiza uongozi wa TANESCO kushughulikia malalamiko aliyopokea kutoka kwa Mbunge wa Muleba Magharibi, Charles Mwijage, kuhusu wananchi walioko visiwani kutozwa gharama kubwa za umeme na wazalishaji binafsi.
“Fanyeni mapitio ya bei. Bei iwe moja; haitakiwi kutofautiana. Kero hiyo kwa wananchi iishe kufikia mwezi Septemba mwaka huu. Ufikapo muda huo, sitarajii kusikia wananchi wa visiwani wakilalamikia tozo kubwa ya umeme unaozalishwa na watu binafsi,” alisisitiza Waziri.
Kuhusu maeneo ambayo umeme umepita juu lakini haujashushwa; Waziri alisema Serikali ilishatoa maagizo kwa mameneja wa TANESCO nchi nzima kuainisha vijiji vyote vyenye changamoto hiyo na kuifanyia kazi, hivyo alimtaka Meneja wa Muleba kushughulikia suala hilo kwa haraka.
Vilevile, Waziri aliagiza wateja wote 5,000 ambao wamelipia umeme katika Mkoa huo lakini bado hawajaunganishwa, waunganishwe ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kutoka hivi sasa.
Waziri alisisitiza viongozi wa taasisi na miradi mbalimbali ya umma kama vile shule, vituo vya afya, nyumba za ibada, masoko, maji na nyinginezo kutenga fedha za kulipia gharama za kuunganishiwa umeme ili huduma hiyo muhimu ipelekwe katika maeneo hayo.