Kikao kazi cha wataalamu wa sheria kutoka taasisi mbalimbali wakiongozwa na Wanasheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria chaanza kazi ya kutafsiri sheria zote nchini.
Kikao kazi hicho cha awamu ya kwanza cha siku 8 kilichoanza kazi Machi 3 kinatarajiwa kukamilisha kazi yake Machi 11 kwa kutafsiri sheria 16.
Huu ni utekelezaji wa agizo lilitolewa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo Prof. Sifuni Mchome Disemba 22, 2020 alipotembelea Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania. Katika ziara hiyo waziri Dkt. Nchemba alisema sheria ni sekta inayomsaidia mtu kupata haki hivyo inapaswa lugha ya Kiswahili itumike kwanza katika masuala mbalimbali ya kisheria kisha lugha nyingine ziwe ni za nyongeza, hivyo sheria, mwenendo wa mashauri na hukumu iandikwe kwa lugha ya Kiswahili ili kuwezesha wananchi kuelewa kwa urahisi kuhusu kesi zao,
Zoezi hili la kutafsiri sheria linategemewa kufanyika kwa awamu tatu kabla ya kuhakikiwa kwa tafsiri hiyo kuangalia kama kilichotafsiriwa ni sahihi na hakijapoteza maana ya kile kilichokusudiwa katika utungwaji wa sheria husika.
Zoezi la kutafsiri sheria linatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2021 ambapo sheria zote nchini zinatarajiwa kuwa zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili.