Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kiwanda cha pamba Ifukutwa Njalu Silanga
Mkurugenzi wa Nondo Investors akimweleza Waziri namna wanavyofanya upakiaji wa unga, na mchele
****************************************
Na. Zillipa Joseph, Katavi
Wawekezaji wa viwanda mbalimbali vya kuchakata pamba, madini na kuongeza thamani mazao ya mpunga; mahindi na alizeti wamelalamikia uwepo wa umeme haba katika mkoa wa Katavi hali inayopelekea kutumia umeme wa jenereta hali inayopelekea kuongezeka kwa gharama za uzalishaji
Wakitoa malalamiko yao kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo wawekezaji hao wamesema wanatumia gharama kubwa ya mafuta kutokana na kutumia mashine za kuzalisha umeme
Bwana Raymond Kamtoni ni Mkurugenzi wa kampuni ya Nondo Investers iliyopo katika manispaa ya Mpanda, inayojishughulisha na upakiaji wa mchele, unga,na ukamuaji wa mafuta ya alizeti ambaye ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama za umeme kwa wenye viwanda vidogo wanaoongeza thamani ya mazao
Kwa upande wake Afisa Mahusiano wa mgodi wa Katavi Twalib Abdallah ameiomba serikali kutengeneza barabara yenye urefu wa kilometa nane ya kuingia mgodini kutokana na barabara hiyo kuwa mbovu na mgodi huo ukiwa ndani ya hifadhi yam situ wa Msaginya unaosimamiwa na TFS
Aidha ameiomba serikali kufikikisha umeme wa gridi mkoani Katavi ili kuondokana na gharama kubwa za mafuta wanazotumia
‘Kwa sasa tunatumia megawati saba za umeme wakati Mpanda pekee inatumia megawati zisizozidi tano hivyo mheshimiwa waziri utaona ni kwa namna gani tunalazimika kutumia mashine zetu wenyewe kuzalisha umeme’ alisema Twalib
Naye bwana Njalu Silanga Mkurugenzi wa kampuni ya NGS wachakataji wa pamba katika Wilaya ya Tanganyika amesema kuwepo kwa umeme haba kunalazimisha kufanya kazi kwa vipindi kutokana na mgao
Unakuta katika shifti moja wafanyakazi wanalazimika kufanya kazi kwa masaa mawili na muda mwingi umeme umekatika, hii inaleta hasara kwa sababu lazima uwalipe kwa masaa yote’ alisema Njalu
Amefafanua kuwa hali hiyo inapelekea kutotimiza malengo kwa wakati na kuongeza gharama
Ameongeza kuwa endapo serikali itawaletea umeme wa uhakika wataweza kuongeza uzalishaji kwani wana mipango mingi ikiwemo nay a kuanzisha kiwanda cha kutengeneza nguo
Akijibu malalamiko hayo Meneja wa TANESCO mkoa wa Katavi Mhandisi Said Msemo amesema wanakamilisha njia ya kupitisha umeme wa Gridi ya Taifa
Amesema kufikia mwezi Oktoba mwaka huu umeme wa Gridi ya Taifa utakuwa umefika mkoani Katavi
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amewataka wawekezaji kutokakukata tama kwani Serikali imeweka mazingira rafiki kwa wawekezaji
Profesa Mkumbo amesema Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli aliliona hilo na ndio sababu ya kuanzisha mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere