Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Zuwena Omary Jiri akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Yefred Myenzi na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Baraka Kanunga Laizer.
………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
KATIBU Tawala (DAS) wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Zuwena Omary Jiri amewataka viongozi wa Tarafa, kata, vijiji na wananchi mbalimbali kutotegemea nyaraka pekee katika kutatua migogoro ya ardhi.
Zuwena ameyasema hayo wakati akielezea miongozo tofauti ya utatuzi wa migogoro mbalimbali ya ardhi iliyopo kwenye maeneo tofauti ya kata na vijiji vya eneo hilo.
Amesema viongozi wasijikite kwenye nyaraka pekee kwani siyo sifa ya kumiliki ardhi ili hali nyingine huwa siyo halali japokuwa nyaraka ni kielelezo kimojawapo cha umiliki wa ardhi.
“Tunapaswa kwenda mbali zaidi ya kumiliki nyaraka na kudhibitisha kuwa anamiliki eneo la ardhi hiyo japokuwa hatupingi kuwa na nyaraka ndiyo kutokuwa na ardhi ila siyo kigezo cha udhibitisho pekee,” amesema Zuwena.
Amesema jambo limefanyika vijijini kisha mtu anakimbilia wilayani kuwa ana nyaraka za umiliki wa ardhi hivyo jamii inapaswa kushirikishwa ili mtu asinyang’anywe ardhi yake kwa nyaraka za kughushi.
Amesema mambo mengi yanatokea kwenye vitongoji na vijiji kisha watu wanafika makao makuu ya wilaya na kulalamikia kuwa wamenyang’anywa ardhi ili hali wananchi ndiyo wanatambua hali halisi ilivyo.
“Kuna watu wameishi miaka mingi kwenye vitongoji na vijiji hao wanapaswa kushirikishwa ili waeleze wanachotambua juu ya hilo na siyo kutegemea nyaraka pekee,” amesema Zuwena.
Amesema wazee wa kimila au watu walioishi miaka mingi wanafahamu wamiliki halisi wa ardhi kwenye vijiji vyao tofauti na mtu akiwa na nyaraka zake ambazo amezipata kwa ujanja ujanja.
Mkazi wa kata ya Naberera, John Peter amesema ni ushauri mzuri umetolewa na kiongozi huyo hivyo viongozi wa ngazi hizo na wananchi kwa ujumla wanapaswa kutekeleza hayo.
Amesema viongozi na wananchi walioishi muda mrefu wakishirikishwa kutakuwa na tija zaidi tofauti na kutegemea nyaraka pekee ambayo imekuwa inachochea migogoro ya ardhi.