Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nasomba katika kata ya Nalasi Mashariki wakiwa katika foleni ya kuchota maji ya bomba hii ikiwa ni mara ya kwanza kijiji hicho kupata maji ya Bomba tangu nchi ilipopata Uhuru mwaka 1961, kwenye mradi wa maji uilotekelezwa na Serikali kupitiaWakala wa usambazaji maji vijijini Ruwasa wilaya ya Tunduru.
Picha na Muhidin Amri,
…………………………………………………………………………………………..
Na Muhidin Amri,Tunduru
KATIKA hali isio ya kawaida,mkazi wa kijiji cha Nasomba Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma Hawa Said anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 67-70 amepoteza maisha akiwa katika foleni ya kusubiri kuchota maji katika moja ya vituo vya kuchotea maji viivyojengwa na wakala wa usambazaji maji vijijini (Ruwasa).
Hawa,alipoteza maisha kwa kile kinachodaiwa ni mstuko baada ya kushuhudia kwa mara ya kwanza maji ya bomba katika kijiji hicho ambacho hakijawahi kupata mtandao wa maji safi na salama tangu uhuru wa Tanganyika na hatimaye Tanzania mwaka 1961.
Badala yake wananchi wa kijiji hicho walilazimika kutumia maji ya mto maarufu wa Ruvuma unaopatikana umbali wa km 3 ambayo hata hivyo hayakuwa salama kwa matumizi ya binadamu kutokana na kutumia pamoja na wanyama wa porini.
Mashuhuda ya tukio hilo akiwemo Diwani wa kata ya Nalas Mashariki Mohamed Mlehani walisema,kabla ya kupoteza maisha Hawa alianguka na kupoteza fahamu akiwa katika foleni na wananchi wengine ndipo alipokimbizwa katika zahanati ya Nasomba kwa ajili ya kupatiwa matibabu kabla ya kufikwa na umauti.
Mlehani alisema, marehemu alipata mstuko kutokana na furaha kubwa aliyonayo mara baada ya kushuhudia maji ya bomba,katika mradi uliotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira Ruwasa wilaya ya Tunduru.
Meneja wa wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Primy Damas alisema, zaidi ya wananchi 13,279 wa vijiji viwili vya Nasomba kata ya Nalas Mashariki na Mbesa kata ya Mbesa wilayani Tunduru, wameanza kunufaika na miradi ya maji iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 253,117,473 zilizotolewa na wizara ya maji.
Damas alisema,miradi hiyo yote imekamilika kwa zaidi ya asilimia 100 na na wananchi wameanza kupata huduma ya maji safi na salama kwenye maeneo yao.
Damas alisema, mradi wa maji kijiji cha Nasomba umetekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 150,554,761 zilizotolewa na Benki ya Dunia ambapo zaidi ya wakazi 3,500 wamenufaika,ulianza kujengwa mwezi mei 2020 na kukamilika Desemba 2020 kwa kuwatumia mafundi wadogo(local fundi).
Alisema, katika mradi huo kazi zilizopangwa kufanyika na zilizofanyika ni kujenga tenki la juu la ujazo wa lita 50,000,nyumba ya mitambo,ununuzi wa mabomba zenye ukubwa tofauti za umbali wa mita 3,200 na viungio vyake.
Damas alisema, kazi zingine zilizofanyika ni ununuzi na ufungaji wa nishati na mfumo wa umeme wa jenereta,ununuzi na ufungaji wa pampu kwa ajili ya kisima,uchimbaji mitaro,ulazaji mabomba na ufikiaji mitaro na kujenga vituo 8 vya kuchotea maji.
Aidha, mradi wa maji Mbesa ulitengewa shilingi milioni 102,562,712 ambazo zinaendelea kutumika kwa ajili ya kuwaondolea kero ya maji takribani wakazi wapatao 9779 wa kijiji hicho.
Alisema, kukamilika kwa miradi miwili ya Nasomba na Mbesa na ile inayoendelea kutekelezwa na wakala wa maji vijijini na usafi wa mazingira Ruwasa kwa ujumla inalenga kuhakikisha huduma ya maji inafika karibu na wananchi,kuchochea shughuli mbalimbali za maendeleo na kumtua mama ndoo kichwani.
Alisema, katika bajeti ya mwaka huu wizara ya maji imeipatia Ruwasa wilaya ya Tunduru kiasi cha shilingi bilioni 2,582,124,451.2 kwa ajili ya kukamilisha na kujenga miradi katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Kwa mujibu wa Damas fedha za mfuko wa P4R shilingi ni 1,366,865,340, mfuko wa PbR -111 shilingi 209,347,963,mfuko wa PbR IV shilingi 337,174,313, na mfuko wa maji wa Taifa shilingi 668,736,835.20.
Amewataka wananchi kutunza miradi hiyo, kuchangia huduma na kutumia maji ya bomba kwa shughuli mbalimbali, badala ya kuendelea na tabia ya kwenda mtoni au kutumia visima vya asili ambavyo hakuna maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
Diwani wa kata ya Nalasi Mashariki Mohamed Mlehani alisema, katika kata ya Nalas kuna vijiji vinne na kijiji cha Nasomba ndiyo kijiji cha kwanza kupata maji ya Bomba yaliyoletwa na Ruwasa.
Alisema, kijiji cha Nasomba kulikuwa na shida kubwa ya maji ambapo wananchi wake walilazimika kutumia umbali mrefu kutembea umbali wa km 3 hadi mto Ruvuma na km 5 hadi mto Luhuwingu kuchota maji kwa matumizi yao ya kila siku.
Mlehani alieleza kuwa,vijiji vilivyobaki vina maji ya kupitia visima vifupi na virefu vilivyochimbwa na taasisi mbalimbali za dini na Halmshauri,hata hivyo bado yanayopatikana bado hayatoshelezi kulingana na idadi kubwa ya watu.
Mkazi wa kijiji hicho Ali Halifa ameishukuru serikali kupitia wizara ya maji kutekeleza mradi wa maji katika kijiji hicho ambao umemaliza shida na mateso ya muda mrefu waliyopata wananchi kutokana na ukosefu wa maji safi na salama.
Alisema, akina mama ndiyo waathirika zaidi wa changamoto ya maji kwakuwa walilazimika kuamka saa 10 usiku kwenda kuchota maji mto Ruvuma na kwenye visima vya asili licha maji hayo kutokuwa safi na salama hasa wakati wa masika.