……………………………………………………………………………
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ameziagiza halmashauri zote nchini zenye maeneo ya kumbukumbu za Historia ya Ukombozi yatunzwe kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadae.
“Natoa maagizo kwa Halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma na halmashauri zote nchini, zitunze maeneo haya ya Urithi wa Ukombozi na mimi nitaenda kila Halmashauri kuhakikisha maeneo kama haya tunayatunza na kuyahifadhi” Waziri Bashungwa yupo mkoani Ruvuma kwenye ziara ya kikazi ambapo leo Februari 26, 2021 ametembelea maeneo ya Urithi wa Ukombozi wa Africa katika wilaya ya Tunduru kata ya Masonya mkoa wa Ruvuma.
Moja ya eneo alilolitembelea ilikuwa kambi ya mafunzo ya kijeshi ya wapigania uhuru wa msumbiji chini ya Samora Machel. Waziri Bashungwa alitembelea nyumba aliyokuwa akifikia Samora Machel pamoja na nyumba aliyokuwa akifikia Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Akiwa Wilayani hapo Mhe. Bashungwa alipokewa na Uongozi wa wilaya hiyo wakiongozwa na Bi. Mwajuma Abbasi Nasombe pamoja na wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama wilayani hapo.