Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (wa nne kutoka kushoto) akiangalia namna ya mitambo inavyofanya kazi wakati kupima tanki la mafuta katika Kituo cha Misugusugu kilichopo Kibaha Mkoani Pwani
Mitambo ya kupima tanki la mafuta katika Kituo cha Misugusugu kilichopo Kibaha Mkoani Pwani
Mtambo wa kupima mita za umeme ulipo katika kituo cha Misugusugu kilichopo Kibaha Mkoani Pwani. Afisa Mwandamizi wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) Bw. Hashim Athumani (wa pili kutoka kushoto) akimuelekeza jambo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (wa kwanza kutoka kulia) namna mitambo inavyofanya kazi wakati kupima mita za maji katika Kituo cha Misugusugu kilichopo Kibaha Mkoani. Pwani.
****************************************
NA NOEL RUKANUGA, PWANI.
Watendaji wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) wametakiwa kusimamia kwa uadilifu Kituo cha Upimaji cha Misugusugu ambacho serikali imewekeza shilingi bilioni 9 kwa ajili ya kutoa huduma ya kupima ujazo wa tanki ya gari yanayobeba mafuta, upimaji wa mita za maji pamoja na umeme.
Kituo hicho cha Misugusugu kilichopo Kibaha Mkoani Pwani ambapo serikali imefanikiwa kufunga mitambo ya kisasa yenye uwezo kutoa vipimo sahihi kwa wakati na ufanisi mkubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mkoani Pwani wakati akifanya ziara katika kituo hicho, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe, amesema kuwa wakala wa vipimo wameendelea kufanya kazi nzuri katika maeneo tofauti.
Mhe. Kigahe amesema kuwa wataendelea kuwekeza katika maeneo tofauti jambo ambalo litasaidia kutoa huduma kwa wakati pamoja na kulinda miundombinu na kuepuka wananchi kununua au kufungiwa vifaa feki.
“Katika mitambo hii tutaweza kutatua tatizo la mita feki za maji na umeme, kwani baada kubainika zitafanyiwa maboresho kabla ya kwenda kutumiwa na wananchi” amesema Mhe. Kigahe.
Amefafanua kuwa kwa siku kupitia mitambo ya kisasa magari 70 ya mafuta yataweza kupimwa jambo ambalo ni uwekezaji mkubwa umefanya na serikali katika kuhakikisha wanatatua changamoto mbalimbali.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe, amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kukagua mradi unavyokwenda, ambapo kwa asilimia kubwa umekamilika.
Prof. Shemdoe amesema kuwa mradi huo una sehemu kuu tatu ambazo ni eneo la kupima ujazo wa tanki la gari yanayobeba mafuta, eneo la kupima mita za maji pamoja umeme.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) Bi. Stella Kahwa, amesema kuwa amefurai ujio wa naibu waziri, kwani amekuja kufatilia uwepo maagizo ambayo tayari wametekeleza.
Bi. Kahwa ameahidi kuendelea kufanya kazi kuwa uadilifu ili kuleta thamani ya mradi kama ulivyokusudiwa, uku akibainisha kuwa mpaka kufikia machi 15 mwaka huu mradi wa kupima mita za umeme utaaza kufanya kazi kwa kasi.