Bw. Ernest Daudi Kaimu Afisa Forodha wa kituo cha Mpaka wa Tunduma akieleza jambo kwa wajumbe wa MAB Wajumbe wa MAB wakifuatilia wasilisho Mpakani TundumaWajumbe wa MAB ambao ni pamoja na Bw. Eric Shitindi ( mwenyekiti- mwenye tshirt nyeupe), Bw. Adam Fimbo ((katibu), Bw. Daudi Msasi, Prof. Said Aboud, Prof. Appolinary Kamuhabwa na CPA Zaina Thabit wakiwa katika picha ya Pamoja mbele ya jengo la Mpaka wa Kasumulu.
Wajumbe wa MAB wakiongozwa na Mwenyekiti Bw. Eric Shitindi katika Mpaka wa Kasumulu, mkoani Mbeya.
************************************
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Afya kwa TMDA (MAB) mnamo tarehe 22 hadi 23 Februari, 2021 wamefanya ziara katika vituo vya forodha vya Tunduma na Kasumulu vilivyoko mkoani Mbeya kwa lengo la kujionea shughuli za udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Akielezea madhumuni ya ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Bw. Adam Fimbo, alieleza kwamba lengo la ziara hii ya wajumbe wa MAB katika vituo vya forodha vya Tunduma na Kasumulu ni mwendelezo wa kuhakikisha wajumbe wapya wa MAB wanapata uelewa wa pamoja juu ya kazi na majukumu ya udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika maeneo mbalimbali ikiwemo vituo vya forodha.
Wakizungumza mbele ya Wajumbe wa MAB kwa nyakati tofauti katika kikao cha pamoja na wasimamizi wa sheria mbalimbali na watendaji waliopo katika Mipaka ya Tunduma na Kasumulu, Maafisa Forodha, Bw. Ernest Daudi (Tunduma) na Bi. Juliana Mbano (Kasumulu) walieleza kuwa Kituo cha Tunduma kina ukubwa wa kilometa 50 na una vipenyo au njia za panya 250 na kituo cha Kasumulu kina vipenyo 32 jambo ambalo limekuwa likileta changamoto za kiudhibiti kwa bidhaa za magendo.
Aidha, ilielezwa kuwa utendaji katika vituo hivyo umekuwa ni wa ushirikiano zaidi ikiwa ni pamoja na kufanya doria za pamoja kwa kushirikisha wasimamizi mbalimbali wa sheria mipakani.
Naye Mkaguzi wa TMDA katika kituo cha forodha cha Tunduma, Bw. Christian Mbwilo, wakati akiwasilisha taarifa ya udhibiti katika kituo cha Tunduma na Kasumulu alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2019/20 jumla ya shehena 388 zilikaguliwa na kupitishwa katika vituo hivyo viwili vya mipakani ambapo shehena 375 ni kwa kituo cha Tunduma na shehena 13 katika kituo cha Kasumulu.
Akizungumza na Menejimenti ya TMDA na Wasimamizi wa Sheria katika vituo hivyo, Mwenyekiti wa Bodi (MAB), Bw. Eric Shitindi, aliupongeza uongozi wa TMDA kwa kusimamia ipasavyo udhibiti katika vituo vya forodha vya Tunduma na Kasumulu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vitendea kazi muhimu kwa wakaguzi vinakuwepo muda wote.
Pia, Bw. Shitindi aliwapongeza watendaji na wasimamizi wa vituo vya forodha vya Kasumumu na Tunduma kwa kufanya kazi kwa ushirikiano jambo ambalo alieleza ndiyo adhma ya Serikali hii ya awamu ya tano chini ya Uongozi wa Rais John Pombe Magufuli katika kufikia lengo la kuhudumia wananchi.