Benki ya NMB imeendelea kupanua wigo wake kwa kufungua tawi ‘NMB SUA’ katika Chuo Kikuu Cha Sokoine Mkoani Morogoro. Ufunguzi wa tawi hili umeleta ahuweni kwa wakazi waliokuwa wanasafiri umbali wa kilomita 6 kwenda matawi ya mjini Morogoro kupata huduma za kibenki.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa tawi hilo, Makamu Mkuu wa Chuo Cha Sokoine Cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda – amesema tawi hilo limekuwa likisubiriwa kwa hamu sana kwani NMB ndio taasisi ya kwanza kufungua tawi maeneo hayo na chuoni hapo ambapo anaamini, litachochea ukuaji wa uchumi na maendeleo katika eneo hilo.
Makamu Mkuu wa Chuo Cha SUA – Prof. Raphael Chibunda akikata utepe kuzindua rasmi Tawi la NMB SUA. Wakishuhudia kutoka kulia kwake ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB – Filbert Mponzi, Meneja wa Kanda ya Mashariki wa NMB- Dismas Prosper, Afisa Mkuu Rasilimali Watu wa NMB – Emmanuel Akonaay na Meneja wa Tawi la SUA – Witness Mwanga.
Chibunda alisema kuwa Benki hiyo licha ya kukuza uchumi pia itawapunguzia gharama, wateja wake
hususani wafanyakazi wa SUA, wanafunzi na wakazi wa Magadu, Mzinga, Kididimo,Misufini, Vibandani, Kasanga, Lugala na Mafiga waliolazimika kusafiri hadi Tawi la Wami zaidi ya kilometa 6 kupata huduma za kibenki- kwani sasa watapata huduma hizo kwa ukaribu zaidi.
Naye Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB – Filbert Mponzi, alisema kufungua tawi hilo litawanufaisha wateja wao ambao ni wanafunzi na wana Morogoro kuweza hufurahia huduma bora za benki hiyo ikiwemo, akaunti ya Mwanachuo, NMB Mkononi, Akaunti ya Fanikiwa, Huduma za bima ikiwemo Dunduliza, akaunti za kilimo na nyingine nyingi.
Ufunguzi wa tawi hili, unafanya Morogoro kuwa na matawi ya NMB 14 na Kanda ya Mashariki matawi 22 na jumal ya matawi 227 nchi nzima!
Sambamba na uzinduzi huo, NMB imetoa msaada wa vifaa vya hosipitali ya SUA na madawati kwa Shule ya Sekondari SUA vyote vikiwa na thamani ya Sh. 13.7 milioni ikiwa ni sehemu ya kurudisha faida kwa jamii.
Uongozi wa Benki ya NMB ukikabidhi vifaa vya hospitali kwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu SUA – Prof. Raphael Chibunda pamoja na daktari wa hospitali ya SUA.
Makabidhiano ya Madawati kwa Shule ya Sekondari SUA.