Meneja wa Sarafu BoT Bw.Ilulu Said akiwasilisha mada katika semina ya Waandishi wa Habari za Fedha, Uchumi na Biashara Mkoani Mtwara.
*************************************
Benki Kuu ya Tanzania BOT imezitaka Benki na Taasisi za Fedha nchini, kutumia noti safi kwenye mzunguko wa fedha na kuziwasilisha zilizochakaa kwenye Benki hiyo ili ziteketezwe, hatua ambayo inalenga kuimarisha zaidi mfumo wa usambazaji wa fedha katika sekta ya hiyo ambayo ni muhimili muhimu wa kiuchumi.
Benki hiyo pia imewataka Wananchi kuwasilisha noti chafu kwenye benki za Biashara ambao nao wataziwasilisha noti hizo BOT Kwa ajili ya kuziteketeza.
Akizungumza katika semina ya Waandishi wa Habari za Fedha, Uchumi na Biashara Mkoani Mtwara, Meneja wa Sarafu wa BOT Bw. Ilulu Said Ilulu amesema fedha zinazotakiwa kuwa kwenye mzunguko zinatakiwa kuwa safi wakati wote ambapo pia amewataka Wananchi kuzitunza fedha zao ili zisichakae haraka.
“Naomba nizitake Benki za Biashara nchini, zipokeeni na zichambueni fedha, zile ambazo ni chafu tuleteeni, sisi BOT kwa ajili ya kuziteketeza” amesema.
Amesema wajibu wa benki hiyo ni kutengeneza, kusambaza na kuharibu sarafu ambapo imebainika imebainika kuwepo kwa Mabenki yanayoingiza fedha katika mzunguko kupitia wateja wao hivyo kuvunja sheria ya usambazaji wa fedha chafu sokoni.
Alibainisha kuwa Benki zote za Biashara zimepewa mamlaka na BoT ya kutoa huduma za kubadilisha noti mbovu na hivyo wananchi wanapaswa kutumia huduma hiyo iliyoanza Mei 27, 2015.
Kuhusu biashara ya kubadilisha fedha kwenye vituo vya daladala Bw. Ilulu amesema wanaofanya biashara hiyo wanakiuka sheria na kwamba kazi hiyo inatakiwa kufanywa na mabenki.
“Kwa wafanyabiashara wakubadilisha fedha kwenye vituo vya daladala na wanaotoa matangazo mitaani ya kuuza fedha chakavu hawa wote wanakiuka sheria, hiyo sio kazi yao, ni kazi ya mabenki ya Biashara” alisema.