Dkt. Gwajima akiangalia dawa aina ya FUKIZA UDANOL na Uzima ambazo zinazalishwa na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na kusisitiza kuimarisha ushirikiano na vyuo vikuu ili kuendeleza tiba asili pamoja na utafiti wa bidhaa hizo nchini
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima leo amemtembelea mzalishaji wa mafuta Tete ya Bupiji na mashine ya kujifukiza iliyopo ofisi ya SIDO jijini Dar es Salaam pamoja na kutembelea ofisi hiyo Waziri Gwajima aliingia Kwenye mashine hiyo na kujifukiza
……………………………………………………………………………………….
Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dar es Salaam.
“Tiba asili ilikuwepo tangu muda mrefu toka miaka ya 1990 na ilishaandikwa kwenye maandiko ya wizara pamoja na Sera ya Afya ya mwaka 2007 hivyo bidhaa zote zilizotengenezwa na wataalamu wa tiba asili ni kuwa na nia ya kuitafuta tiba kama nchi kwa njia yeyote”.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima mara baada ya kuwatembelea wazalishaji wa bidhaa za tiba asili za NIMRCAF, Uzima Herbar Drops, FUKIZA UDANOL, Bingwa Mixed Spices pamoja na Bupiji zote za jijini Dar es Salaam.
Dkt. Gwajima amesema kwamba umefika wakati sasa wa kuzalisha kwa pamoja ili kuweza kuitendea haki ilani ya uchaguzi kwa kuwa na viwanda na kufanya utafiti kwa kuinua bidhaa za tiba asili nchini.
“Lazima tuhitaji mkono wa vyuo vikuu ili kwenda kama timu badala ya kubeba suala la nchi kama la wizara moja, nyinyi UDSM mnashirikiana vipi na China? lazima tuwe na kamati ambayo itatufanya tukimbie haraka ili kuwa na jukumu la pamoja la tiba asili katika kuzuia magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza ili tuweze kufikia faida ya kiafya na ya kiuchumi”. Alisisitiza Dkt. Gwajima.
Aidha, amesema changamoto ya kupumua zinawapata watu wengi hivyo nchi inatakiwa kuwafika wananchi wote na kwa rika zote kuanzia watoto wa shule ya msingi ambapo watoto wajengewe mazoea na uelewa kwamba lishe bora ni ipi na msingi wake uanzie toka utotoni.
“Ninawatambua wazalishaji wote wa tiba asili na watoa huduma ambao wamesajiliwa na Baraza la Tiba Asili/Mbadala, tutaendelea kuwatembelea wote kisha tutakuja na kikao cha kujumuisha mafanikio na changamoto zote pamoja na vyuo vyetu vikuu ambavyo vinafanya utafiti na taasisi zetu ili tuwe na njia ya kwenda mbele na kwa haraka pamoja na tutekeleze ilani ya Uchaguzi ya kuwa na viwanda vya kuzalisha tiba asili na kuwa na utafiti endelevu unaotafiti mimea yetu ya nchi iliyobeba Baraka za tiba asili ili watanzania wanufaike”. Aliongeza Dkt. Gwajima.
Hata hivyo Dkt. Gwajima amewapongeza wazalishaji wote wa tiba asili nchini na kuahidi Serikali inawaunga mkono kwa juhudi wanazofanya na hivyo itasaidia kuleta mapinduzi ya tiba asili nchini.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) Prof. William Anangisye amesema chuo chake kipo tayari kusaidia tafiti mbalimbali ili kuwe na matokeo chanya kwani wao wanamilikiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo matarajio yao ni kuongeza thamani ya tiba asili.
Kwa Upande wa mzalishaji wa mafuta tete ya Bupiji George Buchafwe amesema mashine ya kujifukiza (SAUNA) inasaidia watu wote wanaumwa hata wasioumwa kwani huduma hiyo inasaidia kutoa jasho ambalo limebeba sumu na hivyo kumfanya mtu kumjengea kinga ya mwili na lengo ni kufanya taifa lenye watu wenye afya njema.
Wakati huo huo Mkuu wa kitengo cha Habari na Uhusiano kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Aminieli Aligaesha amesema kuwa hospitali yao inatambua umuhimu wa tiba asili na hivyo imeamua kuchukua mashine ya kujifukiza kwa ajili ya wagonjwa wao ambao wamekuwa wakihitaji huduma licha ya kuwa wakipatiwa huduma za kibingwa kwenye hospitali yao.
Aligaesha amesema kuwa hospitali yao itaweka sifa na viwango gani vya mtu kuingia kwenye mashine hiyo kwakuwa huduma hiyo itakua kama nyongeza katika kuwahuduma wananchi wanaofika kupata hduma kwenye hospitali yao.
Hospitali ya taifa muhimbili imenunua mashine zipatazo nne ambazo tatu zitafungwa kwenye tawi la Upanga na moja Tawi la Mloganzila ambapo mashine hiyo inatarajiwa kufungwa mwishoni mwa wiki hii.