*****************************************
Katibu Tawala wa Wilaya ya Rungwe Bw. Mnkondo Bendera amelipongeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa jitihada inazozifanya za kuwafikia wajasiriamali na wananchi kwa ujumla na kuwapatia elimu ya viwango na uthibitishwaji wa ubora wa bidhaa. Elimu hiyo itawawezesha kuzalisha bidhaa kwa kufuata viwango na zenye ubora na na hivyo basi wateja wao kutumia bidhaa bora na salama sambamba na thamani ya fedha wanazotumia kununulia bidhaa hizo.
Bw. Bendera ametoa pongezi hizo mapema leo alipotembelewa na maafisa kutoka TBS na Wizara ya Viwanda na Biashara wakiongozwa na Meneja Mafunzo na Utafiti Bw. Hamisi Sudi walipofika ofisini kwake kujitambulisha kabla ya kuanza mafunzo kwa wajasiriamali wanaozalisha na kuuza mafuta ya kula wilayani hapa.
Wakati huo huo, Bw. Bendera ameliomba shirika kupanua wigo wa mafunzo ili yawafikie wauzaji wa vyakula maarufu kwa jina la mama na baba lishe (Mama na baba ntilie).Bw.Bendera amesema baba na Mama lishe walio wengi wamekuwa wakipika na kuuza chakula mara nyingi ugali na wali na kuufunika au kufungasha katika mifuko ya nylon (plastics) jambo ambalo linahatarisha usalama wa afya za walaji.
Akilitolea maelezo kuhusu maombi hayo Meneja Sudi alisema Shirika kwa sasa liko katika hatua ya kukamilisha kanuni na taratibu zitakazotumika kuwashirikisha Maofisa wa TAMISEMI .Maofisa hao wanajumuisha Maofisa afya,Biashara na Ustawi wa jamii katika ngazi za halmashauri ili waweze kuwafuatilia kwa karibu na kuwapatia elimu juu ya uaandaji na uhifadhi bora na salama wa chakula.
Aliongeza kuwa tangu mwezi Julai,2019 TBS imeongezewa majukumu yanayotokana na Sheria ya Fedha Na.8 ya Mwaka 2019,ambapo majukumu ya usajili wa bidhaa za Chakula ,Vipodozi na majengo yanayoendeshea Biashara ya bidhaa hizo, yamehamishiwa TBS kutoka iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).