Bibi Elizabeth Msalali Chilingo (90) (aliyeshika  hati
ya ardhi) akiwa kwenye picha ya pamoja
na  Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe.
Dkt. Rehema Nchimbi( mwenye msalaba), Viongozi wa  Wilaya ya Manyoni,wataalam wa ardhi  Mkoa
wa Singida na wanafamilia  mara
baada ya kukabidhiwa hati hiyo ya eneo lake lilichukuliwa na Afisa Ardhi
aitwaye Leonard Msafiri na kisha kupangishwa
kwa Kampuni  mmoja ya simu za
mikono ambapo  Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliagiza  lirejeshwe mara moja  kwa
bibi huyo ambaye ndiye ataingia
mkataba  wa upangaji na
Kampuni  hiyo.

Bibi Elizabeth Msalali Chilingo (90) akitoa shukrani zake kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli  mara baada
ya kukabidhiwa  hati ya eneo lake.

 

Na John Mapepele, Manyoni

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi ametekeleza agizo ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alilomtaka
kushirikiana na Viongozi wa Wilaya ya Manyoni kumrejeshea umiliki  wa eneo  lililokuwa mali ya  Bibi Elizabeth Msalali Chilingo (90) ambaye
lilichukuliwa na Afisa Ardhi aitwaye Leonard Msafiri na kisha kupangishwa  kwa Kampuni  mmoja ya simu za mikono ambayo  imeweka mnara wa mawasiliano lirejeshwe mara
moja  kwa mama huyo ambaye ndiye
ataingia  mkataba  wa upangaji na Kampuni  hiyo.

Akikabidhi  hati ya umiliki wa
ardhi wa miaka 66 wa eneo hilo la Majengo Kiwanja Na 13 hivi karibuni Mkuu wa
Mkoa wa Singida  Mhe, Dkt. Rehema Nchimbi
amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Mhe, Dkt. John Pombe
Magufuli ina dhamira ya dhati ya kuwasaidia wananchi wanyonge ili wapate
haki zao na kuendelea kufanya shughuli zao za maendeleo ili kuchangia katika
uchumi wa kati na hatimaye uchumi wa juu wa Taifa letu.

Amesema Mkoa umejipanga kimkakati kuhakikisha kuwa migogoro yote ya
ardhi inakwisha mara moja  kwenye Mkoa wa
Singida na kuagiza Wakuu wote wa Wilaya na Wataalam wa ardhi  kuanzia sasa kutatua migogoro ya ardhi katika
maeneo husika badala ya kufanya mashauri ya migogoro ya ardhi  maofisini.

“Kuanzia leo sitaki kuona shauri na migogoro ya ardhi ikitatuliwa  maofisini, naagiza wakuu wote wa Wilaya
katika Mkoa wangu  na wataalam kwenda
moja kwa moja  kutatua  migogoro ya ardhi ya wananchi  katika maeneo ya migogoro, hatua kali
zitachukuliwa kwa wote ambao hawatatekeleza
agizo hilo” alisisitiza Mhe. Nchimbi

Akizungumzia kuhusu migogoro ya ardhi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya
Manyoni amesema ni lazima iishe mara moja kwa
kuwa Manyoni  ya sasa ni Sebule ya
Makao Makuu ya nchi-Dodoma na kwamba watu kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania
wanakuja Manyoni kwa kuwa kuna maeneo mazuri yenye fursa za uwekezaji hususan
kwenye  viwanda, biashara  na kilimo cha zao la Korosho ambapo kwa sasa
Wilaya hii inaongoza siyo tu Tanzania bali katika  Bara la Afrika kwenye kilimo hicho ambapo
kumekuwa na shamba la pamoja la Kilimo cha Korosho (Block Farming)lenye takribani ekari 25000.

“Haiwezekani Manyoni hii ambayo ni lango la makao  makuu ya nchi ikaendelea kuwa na migogoro ya
ardhi ambapo sasa  ardhi yake imebeba
uwekezaji mkubwa katika nchi yetu” aliongeza Mhe. Mkuu wa Mkoa

 Akipokea hati yake ya umiliki wa
eneo hilo, Bibi Elizabeth Msalali
alimshukuru Rais Magufuli kwa kusaidia kupatikana kwa kiwanja chake
ambapo amesema Magufuli  ameonyesha kuwa
ni Rais anayewapigania  watu masikini na
wanyonge kama yeye hivyo anamwombea kwa Mungu azidi kumbariki katika utumishi
na maisha yake kwa ujumla.

Aidha Mtoto wa pekee wa Bi Elizabeth ambaye ndiye aliyemwomba Mhe. Rais
Magufuli kuingilia kati suala hili Bwana, Adamu Kazimoto alimshukuru na
kumpongeza Mkuu wa Mkoa, Dkt. Rehema Nchimbi kwa kuharakisha  kukamilisha
mchakato wa kupata  hati ya
umiliki wa kiwanja  hicho kwa mama yake
ambapo amesema  mchakato huo umechukua
muda mfupi sana.

“Naomba niwe mkweli kama tungekuwa na fedha ya kulipia  hiki kiwanja
nadhani  ingechukua  siku
moja au mbili tu baada ya agizo la Mhe.Rais maana Kamishina Msaidizi wa
Mkoa wa Singida Dada Shamimu Hoza alikamilisha
utengenezaji wa hati hiyo mara moja baada ya tamko  hilo la Mhe.Magufuli jambo ambalo limetupa
faraja kubwa kwani sasa mama yangu amepata
haki yake” ameongeza Adamu

Akifafanua Adamu amesema suala hili
alianza kufuatilia zaidi ya  miaka
tisa iliyopita, na anamshukuru Rais Magufuli  kwa kutoa suluhisho la kudumu ambapo pia
ameongeza kwamba mgogoro huo umeifanya familia ya Mzee Kazimoto kuwa kitu
kimmoja licha sintofahamu ambazo zilikuwepo hapo awali kwa sababu ya tamaa ya
pesa kwa wanafamilia.

Mhe. Rais John Pombe  Magufuli
alilitoa agizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida kushughulikia mgogoro  huo tarehe 31Januari 2021 aliposimama
kuwasalimu wananchi wa Manyoni wakati akiwa safarini akitokea Tabora kwenda
Dodoma.

Rais Magufuli  alisikiliza  kero inayowakabili wananchi hao ambao
walilalamikia  kitendo cha Idara ya Ardhi
kuchukua maeneo  yao bila kuwalipa fidia  na wengine kuamriwa  kuondoka katika  eneo hilo baada ya kupewa nyaraka  za kupatiwa
radhi(offer) hali iliyozua mgogoro kati ya wamiliki wa asili wa eneo
hilo na Idara ya Ardhi.

Rais ameagiza wananchi wenye offer
waruhusiwe kuendeleza maeneo waliyopatiwa na wamiliki wa asili wa eneo
hilo  kulipwa fidia kwa mujibu wa Sheria.

Awali, kufuatia agizo  la
Mheshimiwa Rais, Timu Maalum ya wataalam kutoka Mkoani na Wilaya ya Manyoni
iliyoongozwa na Kamishina Msaidizi wa Mkoa wa Singida Shamimu Hoza Shaban
ilikutana  familia nzima ya mmiliki wa
asili wa eneo hilo marehemu  Salum
Kazimoto aliyefariki mwaka 1973
ambayo   ilikuwa  inavutana
kuhusu  umiliki wa eneo  hilo ambapo
baada ya  majadiliano ilikubaliana
kwa kauli mmoja kwamba mmliki halali  wa
eneo hilo ni Bibi Elizabeth Msalali.

Kutokana  na  Wilaya ya Manyoni kuonekana kuwa na migogoro
ya ardhi kadhaa ya ardhi kwa muda mrefu sasa, mkakati maalum wa kusikiliza kero
hizo umeandaliwa  ambapo timu ya wataalam
na viongozi wa Halmashauri hiyo unazungukia katika maeneo husika ili
kuhakikisha migogoro yote inaisha  kama
ilivyoamriwa.