Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt Zainab Chaula akizungumza wakati akifunga Mkutano wa Baraza la 27 la Shirika la Posta Tanzania (TPC) uliofanyika jijini Dodoma kushoto ni Naibu wake Dkt Jim Yonazi akisikiliza.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Jim Yonazi (Kulia) akizungumza kabla kufungwa kwa Mkutano wa Baraza la 27 la Shirika la Posta Tanzania (TPC) uliofanyika jijini Dodoma Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Zainab Chaula akisikiliza na Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi na Utawala wa Wizara hiyo Kitolina Kippa akimwangalia kwa makini.
Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi na Utawala wa Wizara Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Kitolina Kippa akiimbisha wimbo wa mshikamano daima kabla ya kufungwa kwa Mkutano wa Baraza la 27 la Shirika la Posta Tanzania (TPC) uliofanyika jijini Dodoma. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Zainab Chaula, akifuatiwa na Naibu wake Dkt Jim Yonazi (Katikati)
Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Hassan Mwang’ombe (Kushoto) akimpokea Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt Zainab Chaula (kulia) kabla ya kufunga Mkutano wa Baraza la 27 la Shirika hilo uliofanyika jijini Dodoma
Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Clarence Ichwekeleza akizungumza na baadhi ya watendaji wa Shirika la Posta Tanzania baada ya kufungwa kwa Mkutano wa Baraza la 27 la Shirika hilo uliofanyika jijini Dodoma
……………………………………………………………………………..
Na Faraja Mpina- WMTH
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Zainab Chaula amelitaka Shirika la Posta Tanzania (TPC) kujitathmini juu ya utekelezaji wa malengo waliyojiwekea katika kipindi hiki cha kuelekea robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2020/2021.
Dkt Chaula aliyazungumza hayo wakati akifunga Mkutano wa Baraza la 27 la Shirika hilo lililofanyika jijini Dodoma la kujadili na kutathmini juu ya utendaji kazi wa Shirika hilo
Ameongeza kuwa katika kipindi hiki cha mwaka ni matarajio Shirika hilo kufikia asilimia 60 ya malengo waliyojiwekea, na kama halijafikia asilimia hizo Shirika linatakiwa kujitathimini na kuelekeza nguvu katika mikoa ambayo haikufanya vizuri ili kuiwezesha nayo iweze kwenda sambamba na matarajio ya Shirika hilo.
Dkt Chaula ameongeza kuwa Shirika la Posta limepata watendaji wabobezi kitaaluma, wabunifu, waadilifu na wenye maadili ya utumishi wa umma ambao wanatakiwa kuwasaidia viongozi wao kwa maendeleo ya Shirika
“Hakuna kiongozi ambaye hawezi iwapo akisaidiwa na watendaji wake, ukiona kiongozi hafai maana yake watendaji anaowaongoza hawamsaidii, hawamshauri na hawatizimi wajibu wao katika utendaji”, Dkt Chaula
Aidha amesisitiza upendo, amani na mshikamano mahali pa kazi kuepusha malumbano na manung’uniko ili kuimarisha utendaji kazi wa Shirika hilo.
Naye Dkt Jim Yonazi Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amempongeza Postamasta Mkuu Hassan Mwang’ombe na watendaji wake kwa kufanya biashara ya ushindani na kuleta matokeo yanayoonekana na kuwaasa watendaji wa Shirika hilo kuendelea kushikamana kwa kufanya kazi kwa juhudi na kujituma.
Awali Postamasta Mkuu Mwang’ombe akitoa taarifa kabla ya kufungwa kwa Mkutano wa Baraza hilo alisema watendaji wa Shirika wamepata mafunzo mbalimbali kupitia Baraza hilo ikiwemo mafunzo ya kuvitambua viashiria hatarishi kwa uendeshaji wa Shirika, namna ya kuviepuka na kuvitatua viashiria hivyo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari