WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuwa somo la Historia ya Tanzania linatarajia kuanza rasmi kufundishwa Julai mwaka huo.
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuwa somo la Historia ya Tanzania linatarajia kuanza rasmi kufundishwa Julai mwaka huo.
Baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo pamoja na waandishi wa habari wakifatilia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako wakati akitoa taarifa kuwa somo la Historia ya Tanzania linatarajia kuanza rasmi kufundishwa Julai mwaka huo.
……………………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imesema tayari imekamilisha kuandaa mihtasari kwa ajili ya somo jipya la historia ya nchi litakaloanza kufundishwa mwezi July 2021, kama alivyoagiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kufundishwa kwa somo hilo kwa madarasa yote.
Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dodoma Waziri wa Elimu Sayansi na Taknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema mara maada ya tamko la Rais kutoka walianza mara moja maandalizi ambapo mpaka sasa wamekamilisha zoezi la kuandaa mihtasari kwa ngazi zote.
” Tangu Rais alipotangaza tamko lile na sisi Wizara ya Elimu tulilichukulia kwa uzito mkubwa na mpaka sasa tayari tumekamilisha mihtasari yote na sasa vitabu vinaandaliwa kwa ajili ya kufundishia wanafunzi na tunatarajia hadi kufikia mwezi marchi vitabu vyote vitakuwa tayari” amesema Prof Ndalichako.
Amesema maandalizi ya vitabu vitakavyotumika katika kufundisha vinaandaliwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwamo wabobevu katika historia ya nchi ya Tanzania.
“Maandalizi haya ya vitabu na historia tunashirikiana na Wadau mbalimbali katika kuandaa vitabu hivi hatufanyi peke yetu tumeshirikisha Wizara mbalimbali na taasisi ili kufanya kwa uhakika zaidi ili somo hili jipya hapa nchini lifundishwe kwa ufasaha mkubwa” amesema.
Amesema nchi ya Tanzania ina historia kubwa sana ambayo ikifundishwa kwa vijana wetu itasaidia kuwa wazalendo na kulinda rasilimali za taifa sambamba na kujua nchi ilipambana vipi katika kupata uhuru wake.
Amebainisha kuwa somo hilo litafundishwa kwa lugha ya kiswahili kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita ili somo hilo liweze kueleweka vizuri kwa wanafunzi pindi wanapolisoma somo hilo la historia ya nchi ya Tanzania.
Amesema kuwa somo hilo rasmi litaanza kufundishwa mwezi july 2021 katika ngazi zote ambapo kwa kidato cha tano watakuwa wakianza masomo na somo hilo wataanza nalo huku madarasa mengine yatakuwa yakianza mhula wa pili wataanza na somo hilo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Taknolojia Dkt Leonard Akwilapo amesema somo hilo litafundishwa kwa lugha ya kiswahili na kwa kidato cha tatu, nne, na sita watasoma tu bila kufanya mitihani ila kwa kidato cha kwanza na kidato cha pili ndio watakao fanya mitihani.