Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani (aliyesimama) akizungumza wakati wa Semina ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, iliyokuwa na lengo la kuieleza Kamati hiyo kuhusu majukumu ya Wizara pamoja na Taasisi zilizochini yake iliyofanyika jijini Dodoma, Februari 11, 2021. Kushoto kwa Waziri ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Leonard Masanja.
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani (katikati mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Watendaji wa Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zilizochini yake, mara baada ya semina iliyotolewa kwa kamati hiyo ili kuieleza kuhusu majukumu ya Wizara na Taasisi zake iliyofanyika jijini Dodoma, Februari 11, 2021.
**************************************
- Matumizi ya mafuta ya ndege yaongezeka
Na Zuena Msuya Dodoma,
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani amesema usambazwaji na upatikanaji wa umeme vijijini umepunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya mafuta ya taa nchini.
Dkt. Kalemani alisema hayo tarehe 11 Februari, 2021 wakati wa semina iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, iliyokuwa na lengo la kuieleza kamati hiyo majukumu ya Wizara pamoja na Taasisi zilizo chini yake.
“Kwa sasa matumizi ya mafuta ya taa yamepungua hadi kufikia takribani lita 110,000 kwa siku tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, ambapo lita zaidi ya 140,000 zilikuwa zikitumika kwa siku na hii inatokana na shughuli nyingi za kijamii vijijini kutumia umeme.” Alisema Dkt.Kalemani
Aliongeza kuwa, mafuta ya taa yalikuwa yakitumika kama chanzo cha mwanga vijijini, ambapo sasa asilimia kubwa ya wakazi wa vijijini wanatumia umeme kujipatia mwanga.
“Sasa hivi matumizi ya mafuta ya taa yamepungua sana na yanaendelea kupungua siku hadi siku, kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya umeme, hii inatokana na juhudi zenu ninyi wabunge pamoja na Serikali kuhakikisha kuwa umeme unasambaa vijijini.” Alisema Dkt. Kalemani
Kuhusu kuongezeka kwa matumizi ya Mafuta ndege, Dkt. Kalemani alisema kuwa kwa sasa matumizi ya mafuta hayo yameongezeka kutokana na kuwepo kwa safari nyingi za ndege zinazomilikiwa na serikali.
Alisema kuwa, kwa sasa Tanzania inamiliki ndege nyingi ambazo hufanya safari zake ndani na nje ya nchi, hivyo kufanya mafuta hayo kutumika kwa wingi.
Alifafanua kuwa, matumizi ya mafuta ya ndege yamepanda hadi kufikia lita Laki Sita kwa siku tofauti na huko nyuma matumizi yalikuwa chini ya Lita Laki Tatu kwa siku.
Katika hatua nyingine, alisema kuwa, Serikali inaendelea na mpango wa kuanzisha vituo vidogo vya mafuta katika maeneo ya vijijini ili kusogeza karibu huduma ya mafuta ya Petroli, Dizeli na Taa.
Alisema kuwa, mpango huo utaondoa adha kwa wananchi kutembea umbali mrefu kufuata bidhaa hiyo, na pia kuondoa hatari inayoweza kuwakumba watu wanaohifadhi bidhaa hiyo ndani ya nyumba zao.
Taasisi zilizo chini ya Wizara, zilizoshiriki Semina hiyo ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Kampuni ya Uendelezaji JotoArdhi Tanzania( TGDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mamlala ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).