……………………………………………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
SERIKALI wilaya ya Kibaha ,mkoani Pwani ,imetoa agizo kwa wavamizi wa shamba la Serikali la Mitamba waondoke mara moja,na kudai kwamba hilo sio shamba la bibi .
Aidha baadhi ya wenyeviti wa Serikali ya mitaa ,wameaswa kuacha kuuza ardhi kwakuwa hawana mamlaka hayo na kukemea wasijaribu kujiingiza kuuza maeneo yoyote .
Akizungumza na baadhi ya watendaji wa halmashauri ya Mji wa Kibaha,madiwani na viongozi wa halmashauri ,mkuu wa wilaya ya Kibaha, mhandisi Martin Ntemo alisema ,shamba la Mitamba bado lina hoja ,kwani kuna watu waliokuwa na malalamiko yao ,ambayo yamefikishwa wizara ya ardhi na orodha yao .
Alieleza, kabla ya majibu yao hajaletwa watu wameanza kuvamia shamba hilo na wengine kuuza vipande kinyume na sheria .
Ntemo alifafanua, wilaya imeshachukua hatua za awali na kuagiza uvamizi usiendelee.
Hata hivyo ,amewatahadharisha wananchi wasiingie katika mikono ya matapeli kuuziwa maeneo kwenye shamba hilo kwani watapata hasara,na kusema atakaetaka eneo aende kwa mkurugenzi kupata ufafanuzi.
“Kutoka hekta 4,100 sasa zimebaki hekta 1,037 na uvamizi bado ni mkubwa ,nawataka wananchi waache mara moja kuvamia maeneo kiholela bila utaratibu kwa kisingizio cha mashamba pori” alielezea Ntemo.
Awali akiibua hoja hiyo na kutaka ufafanuzi ,diwani wa kata ya Mailmoja ,Ramadhan Lutambi alizitaka mamlaka za juu ,kuchukua hatua ili kunusuru shamba la Mitamba ambalo linamegwa siku hadi siku .
Alisema ni jukumu lao kulinda eneo hilo la Serikali na hatua za haraka zichukuliwe ,na majibu yapatikane ili kumaliza mgogoro wa eneo hilo .
Lutambi pia alibainisha kwamba ,mashamba pori yamekuwa kero watu wasihodhi maeneo makubwa pasipo kuyaendeleza na mashamba pori yaliyopo yaorozeshwe na hatua za kupokonywa zichukuliwe .
Nae mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha, Jennifer Omolo alisema wanafanyia kazi tatizo la Mitamba, ambapo taarifa zipo wizara ya ardhi na ameshaandika barua kwa Kamishna ambae anashughulikia mgogoro huo namba 34.
Kuhusu wananchi waliovamia eneo hilo amedai wamepewa notisi ili waondoke .