…………………………………………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
ATHUMANI Nassoro mkazi wa Kijiji cha Dutumi Kata ya Dutumi Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani, amenusurika kuliwa na mamba.
Mkazi huyo aliyekwenda katika mto huo mwishoni mwa wiki, kwa ajili ya kukoga, alipofika akawakuta wadogo zake wa kike wakiwa hapo akawaambia waondoke, kisha akaingia lakini kwa bahati mbaya alipomaliza alisikia kishindo kikubwa nyuma yake, kugeuka akamuona mamba ghafla akamvamia miguuni.
Alisema kuwa alipobaini hatari hiyo alikubali kila kitu kilichofanywa na mamba huyo, ambapo alimzamisha mara mbili kwakuwa ana uzoefu wa kuogelea alibana pumzi, akimuinua juu anapumua, alifanya hivyo mpaka mamba akajua amekufa amamtoa katika maji madogo.
“Aliponitoa pembezoni mwa maji madogo nikakamata matete kwa bahati nzuri akatokea mkazi Ramadhani Michaka akapiga yowe watu wakaja kunisaidia kwa kunivuta mabegani,” Ramadhani.
Alisema kuwa pamoja na watu 15 kutaka kumwokoa lakini walivutwa mpaka majini hali iliyompatia ujasiri wa kuingiza mikono yake ndani ya maji kisha kuukamata mdomo wa mamba ambae alikuwa ameshaing’ata miguu yake yote miwili.
“Nilifanikiwa kuufunua mdomo wake baada ya kuona hivyo akaniacha lakini alikiwa ameshanijeruhi miguu yote miwili alininyofoa nyama za pajani, pia alitenganisha maungio ya mguu wa kulia kati ya paja na kifundo cha goti, nikakimbizwa zahanati ya Kwala baadae Kituo cha afya Mlandizi kabla ya Tumbi,” akisema Mhanga huyo.
Aliongeza kuwa kabla ya tukio hilo babu mjomba wa baba yake ameliwa na mamba, wakamkuta amepoteza maisha, wiki moja iliyopita kuna mkazi mwingine amechukuliwa na mamba mpaka sasa mwili wake haujapatikana wakati siku tatu zizopita mamba amempora dumu shangazi yake aitwae Mama Asha, ikiwa ni harakati za kutaka kumkamata.
Makamu Mwenyekiti Mstaafu Diwani wa Kata ya Ruvu Charles Mwakamo alisema kuwa mamba katika ukanda wa Mto Ruvu wapo wengi, na kwamba wananchi wengi wanapoteza maidha huku wengine wakipatwa na ulemavu wa kudumu.
“Tunaiomba Serikali kupitia Wizara husika kuwavuna mamba katika mto huo, unaopita katika maeneo mbalimbali ya ukanda huu wa Dutumi, Ruvu na maeneo mengine, kipindi kizuri ni hiki kwani ifikapo mwezi wa tatu huenda kumawa na mvua hivyo maji kuongezeka,” alisem Mwakamo.
Aliongeza kwa kusema kuwa kutokana na changamoto hiyo Wizara husika kupitia wataalamu wao wasicheleweshe kibali cha kufanyika kwa zoezi hilo, au kuwapatia ruhusa wananchi kuwauwa pindi wanaposababisha maafa au vifo kwa binadamu.