**************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema juhudi za Serikali za kupambana na
rushwa, kudhibiti upotevu wa mapato, matumizi ya fedha za Serikali na
kusimamia uwajibikaji kwa watumishi wa umma ni sababu zilizowezesha Ofisi ya
Rais pamoja na Ofisi ya Waziri kuaminika zaidi.
Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na viongozi wa Umoja
wa Wanake Tanzania (UWT) akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma.
Amesisitiza kuwa vita dhidi ya rushwa ni endelevu.
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais
Dkt. John Magufuli imepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya rushwa ambapo kwa
Afrika Tanzania inaongoza kwa mujibu wa ripoti ya taasisi ya Transparency
Internation iliyotolewa hivi karibuni.
Ripoti hiyo mpya iliyotolewa Julai 11, mwaka huu inaonesha kwamba kwa sasa
Tanzania inaongoza katika nchi 35 za Afrika baada ya kupungua kwa vitendo vya
rushwa katika sekta nyingi, ambapo Ofisi ya Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu
zimeonekana kuaminika zaidi.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwatahadharisha watumishi wa
umma kwamba Serikali kamwe haitomvumilia mtumishi atakayebainika
anayejihusisha na vitendo vya rushwa na aliwataka wahakikishe kuwa
wanatekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi bila ubaguzi.
Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga vizuri katika mapambano dhidi ya
rushwa, hivyo amewataka wananchi wasisite wakati wote kutoa taarifa kwa
vyombo husika pale watakapobaini uwepo wa watumishi wanaojihusisha na
vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.
“Watumishi wa umma wanatakiwa kutambua kwamba jukumu lao kubwa ni
kuwatumikia wananchi kwa kuzingatia maadili na kanuni za utumishi wa umma
zilizowekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni na si vinginevyo. Serikali hii kamwe
haitowaonea haya au kuwafumbia macho watumishi wa hovyo.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kuwa suala la kuwaondoa kazini watumishi
wazembe, wasiotimiza wajibu wao ipasavyo pamoja na wale wasiozingatia
maadili ya utumishi wa umma ni endelevu kwa sababu Serikali inahitaji watumishi
wa umma wenye heshima na nidhamu ya kazi.
Suala la kuwapokea, kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi katika maeneo
mbalimbali ya kutolea huduma kwa wananchi zikiwemo ofisi za Serikali kuanzia
ngazi ya kijiji hadi Taifa ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya
Tano, hivyo watumishi wa umma wanapaswa kuzingatia jambo hilo.