……………………………………………………………………..
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Walimu wakuu wa shule za msingi wametakiwa kutumia mafunzo waliyoyapata kurekebisha matatizo yaliyopo katika shule wanazoziongoza na sio kusubiri watu wa nje kwenda kufanya kazi hiyo.
Rai hiyo imetolewa na mtendaji mkuu wa wakala wa maendeleo ya uongozi wa elimu(ADEM) iliyo chini ya wizara ya elimu Dkt Siston Masanja wakati akifunga mafunzo ya udhibiti ubora yaliyotolewa kwa walimu zaidi ya 300 kutoka halmashauri 7 za mkoa wa Manyara.
Dkt Masanja alisema ni mategemeo kuwa walimu waliopata mafunzo hayo kwa awamu ya Kwanza wataenda kutumia maarifa hayo katika kudhibiti ubora wa taaluma na maendeleo ya shule kwa ujumla.
Alieleza hawapaswi kwenda kukaa ofisini tuu bali wakafuatilie kila kinachoendelea katika shule zao ikiwemo ufundoshaji ambapo kwa kufanya hivyo ndani ya miezi sita kutakuwa na mabadiliko makubwa.
“Kahakikisheni mnashughulikia yale yote mnayoona mnastahili kwa kufanya maamuzi yatayoleta matokeo chanya na sio mkakae kusubiri watu kutoka nje waje kutatua changamoto wakati nyie mpo na uwezo wa kutatua mnao,” Alisema Dkt Masanja.
Alifafanua kuwa kudhibiti ubora ni pamoja na kurekebisha mambo ndani ya shule zao na kuangalia namna wanavyowaongoza walimu wao kwa kufiatilia kama wanaadaa mpango kazi au wanatumia ya miaka iliyopita na kama hawaandai waangalie ni namba gani wanaweza kuwasaidia ili wanafunzi waweze kupata elimu sahihi na kuweza kuinua kiwango cha elimu.
Mratibu wa mafunzo hayo Malimi Sai alisema kuwa walimu hao wamepata mafunzo juu ya udhibiti ubora wa shule, ufunfishaji, mtaala, ufuatiliaji , tasmini na mengineyo ambapo wanaamini kuwa mafunzo hayo yamewapa umahiri mkubwa wa kwenda kisimamia shule zao.
Kwa upande wake mkuu wa chuo Patandi elimu maalum Lucian Segesela alieleza kuwa wakala wa maendeleo ya uongozi wa elimu (ADEM) ni mkombozi sahihi katika masuala yanahusu udhibiti wa ubora wa elimu kwani hata katika ngazi ya chuo walishapata mafunzo yenye weledi mkubwa kwaajili ya kuimarisha usimamizi.
Nae mmoja wa walimu hao Nyanda Steven kutoka halmashauri ya mbulu alisema kuwa mafunzo hayo yameweza kuwanufaisha kwani wamegundua kuwa wao ni wadhibiti namba moja katika maeneo ya shule ambapo wamejua kuwa wanafunzi, walimu,wazazi na jamii kwa pamoja wanaweza kutoa tathimini zinazoweza kuboresha shule.
“kwa kweli mafunzo haya ni mazuri yatatusaidia kuboresha shule kwanzia ngazi kata hadi taifa na hata kwa wale wenzetu ambao hawakupata haya mafunzo tutaenda kuwafundisha na wao ili kiwango cha elimu kiweze kuinuka,” alisema mwaalimu Nyanda.
Hata hivyo mafunzo hayo yanefanyika katika Chou cha ualimu Patandi Mkoani Arusha kwa mada wa siku tatu.