***************
NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ,Kitongoji cha Nyakahamba ,kata ya Kerege Frenk Masihaga na wakazi wengine 300 wa kitongoji hicho wamekihama chama hicho na kurudi CCM ,ili kuunga mkono juhudi za serikali na maendeleo yanayoletwa kwa kasi na Rais dk.John Magufuli.
Akipokea wanachama hao ,katika ziara yake ya kufanya vikao vya ndani kukosoana na kuwekana sawa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa,vitongoji ,huko Kerege Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Bagamoyo,Alhaj Abdul Sharif alisema, wamerejea CCM wakati muafaka.
“Hamjafanya makosa kurudi kwa Chama dume ,ila mkafanye kazi ya CCM Nyakahamba kuhakikisha CCM inarudi madrakani na kukikomboa kitongoji hicho”alisema alhaj Sharif.
Hata hivyo alieleza, wanachama waonyeshe ushirikiano ,waondoe makundi na kukisemea Chama na serikali kwa yale yanayofanyika.
Sharif alielezea kwamba, mkakati uliopo kiwilaya ni kujipanga kushinda uchaguzi nafasi zote na ndio maana yupo katika ziara ya vikao vya ndani kurekebishana wenyewe na kurejesha wanachama ndani ya chama kwani mtaji wa chama ni kuongeza wanachama.
Alifafanua ziara yake imezaa matunda tayari kwa maeneo ambayo ameshapita ikiwemo Kibindu wapinzani 200 wamerudi CCM akiwemo mwenyekiti na diwani waliogombea uchaguzi uliopita.
Kata ya Talawanda wapinzani wawili,Mandela wanne akiwemo aloyegombea udiwani uchaguzi mkuu uliopita na kata ya Mkange watano.
Sharif alielezea,ni wajibu wa kila kiongozi wa shina,tawi,kijiji,kitongoji na kata kusimama imara ,kujipanga ili kupambana CCM iweze kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa na vitongoji 2019 na uchaguzi mkuu ujao 2020.
Awali mwenyekiti wa kitongoji cha Nyakahamba Masihaga alisema, kitongoji hicho kina wakazi 420 ambapo ameondoka na wakazi 300 .