***********************************************
Na Atley Kuni, Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amewapa wiki mbili Viongozi wa Sekretarieti za Mikoa, na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa ndani ya wiki mbili kuanzia sasa wawe wamesimika mfumo wa kutambua orodha ya majengo na mabango yaliyopo katika maeneo yao ili kurahisisha ukusanyaji wa kodi na ushuru.
Akizungumza wakati wa kikao kilicho wakutanisha, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini leo jijini Dodoma, Mhe. Jafo amesema, changamoto kubwa ambayo inasababisha zoezi la ukusanyaji kodi za majengo ni kutokuwepo kwa orodha kamili ya majengo katika mamlaka husika.
Hivyo, amesema suluhu ya kudumu itakayosaidia kuyabaini kwa wepesi na kurahisisha ukusanyaji wa kodi za majengo na ushuru wa mabango ni kuwepo kwa mfumo utakaosaidia kuyabaini majengo yote na mabango na kuhifadhi kumbukumbu hizo katika Kompyuta.
“Tunataka kuanzia tarehe 05 hadi 28 Februari, 2021, iwe ni kazi ya kubainisha majengo yote yanayopaswa na ambayo yanakidhi kulipiwa kodi,” amesema Waziri Jafo na kuongeza kuwa nyumba za matope zimeondolewa katika utaratibu huu.
“Kila Mtendaji wa Mtaa, Mwenyekiti wa Kijiji anatakiwa kuwa na takwimu za majengo yote yanayopaswa kulipiwa kodi, Mkurugenzi hakikisha kuwa Mtendaji wako wa Kijiji au Mtaa anakupatia takwimu ndani ya Wiki mbili kuanzia leo,” alisisitiza Mhe. Jafo.
Waziri Jafo amesema, Wakurugenzi wa Halmashauri watatakiwa kuwasilisha kanzi data hizo ngazi ya Wilaya kwa ajili ya uhakiki kwa Mkuu wa Wilaya, kabla ya kuwasilisha ngazi ya Mkoa kwa Katibu Tawala wa Mkoa na ifikapo tarehe 04 Machi, 2021 zoezi hilo liwe limekamilika na taarifa ya majumuisho iwe imetumwa kwa Katibu Mkuu TAMISEMI.
Waziri amesisitiza kuwa, taarifa hizo zitatakiwa kuanisha nyumba, mmiliki na mawasiliano yake kwa wepesi wa rejea, ambapo mara baada ya hapo, itafanyika kampeni maalum ya kuanza kukusanya kodi ya majengo nchi nzima, itakayoanza tarehe 22 Machi hadi tarehe 05 Aprili, 2021.
“Tunataka huko mbeleni hizi Mamlaka za Serikali za Mitaa ziweze kufanya baadhi ya shughuli za Maendeleo zenyewe, hivyo katika zoezi hili tutaweka mfumo maalum utakaoweza kuona mambo kadhaa yanayo endelea nchi nzima kwenye kazi hii, hatutaki watu washindane bali tunataka kila Halmashauri iwe ya kwanza,” amesema Mhe. Jafo.
Kuhusu vitambaulisho vya wajasiriamali, Waziri Jafo, amesema tayari vitambulisho million 1.6 vimechapishwa na mamlaka ya Mapato Tanzania na kusambazwa katika Mikoa.
“Huu ndio mwanzo na maelekezo ya Serikali, ambayo yatakuwa katika makundi matatu, Wafanya Biashara wakubwa wanaolipa kodi TRA, Wafanyabishara wa kati wenye Leseni za Halmashauri na kundi la tatu ni wenye Vitambulisho vya Mjasiriamali, kila mmoja wetu lazima awe sehemu ya kundi moja wapo” amesema Waziri Jafo
Amesema kuwa asiyekuwa na kitambulisho au hana kundi lolote kati ya hayo, asiruhusiwe kufanya biashara.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Aldolf Ndunguru amesema pamoja na kwamba zoezi la kukusanya kodi hizo limehamishiwa Mamlaka za Serikali za Mitaa bado anaamini ushirikishwaji madhubuti wa viongozi katika maeneo mbali mbali utawezesha kukabiliana na mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali.
Akitoa salamu za Mamlaka ya Mapato nchini, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini TRA, Dkt Edwin Mhede, ametaka kuwepo ushirikiano na Wakuu wa Wilaya kwani maeneo hasa ya upande wa forodha bado hali siyo nzuri kama matarajio na malengo yao yalivyo, hivyo akaomba msaada wa karibu kutoka kwa viongozi hao ambao ni wenyeviti wa Kamati za ulinzi za Wilaya.