Na Mbaraka Kambona, Dodoma
TAASISI za fedha nchini
zimeipongeza Serikali kwa maamuzi ya kulifufua Shirika la Uvuvi Tanzania
(TAFICO) na kulipa tena nafasi ya kuweza kusimamia mnyororo wa thamani wa zao
la Samaki huku wakiahidi kutoa mtaji ili kuliimarisha shirika hilo.
hayo yalisemwa na
Mkurugenzi Mtendaji, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Japhet Justine alipokuwa
akiongea na Waandishi wa Habari muda mfupi baada ya kumaliza kikao kazi cha
kujadili maeneo ya uwekezaji ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kilichofanyika
jijini Dodoma Februari 2, 2021.
Akiongea kwa niaba ya
Viongozi wengine wa taasisi za fedha waliohudhuria kikao hicho, Justine alisema
kuwa TAFICO ni shirika kubwa linaloshikilia mnyororo mzima wa thamani wa samaki
hivyo kufufuliwa kwa shirika hilo kutawasaidia wavuvi kuwa na masoko ya
uhakika.
“Tunaipongeza Serikali kwa
maamuzi haya makubwa ya kulifufua shirika hili, na sisi tumewahakikishia kushirikiana
nao katika kutoa mitaji ambayo itaanzia kwa TAFICO yenyewe na wale wote
wanaojihusisha katika mnyororo huu wa thamani ikiwemo wavuvi, wasafirishaji na
watengeneza barafu,” alisema Justine.
Alisema kwa sasa kuna
wananchi zaidi ya laki mbili (200,000) wanaojihusisha na uvuvi na kuongeza kuwa
hao wote wataenda kuwafungamanisha katika mnyororo huo wa thamani.
Aliongeza kuwa kufufuliwa
kwa shirika hilo kutaongeza fedha za kigeni, uhakika wa kupata masoko makubwa
ya kimataifa ambayo yataleta mikataba ya kibiashara itakayowarahisishia wadau
walioko katika sekta ya uvuvi kukopeshwa mitaji.
“Tunaamini mabenki ambayo
yalikuwa yanapata shida kupata mikataba ya kuweza kuwapatia wafanyabiashara
wadogowadogo mitaji, sasa kwa kupitia mikataba ya TAFICO italeta ahueni kubwa
na kupunguza madhila yaliyokuwa yanazuia mabenki kutoa mitaji,” alifafanua
Justine.
“Sisi kama taasisi za fedha
ikiwemo mabenki, Kituo cha Uwekezaji na Mifuko ya Pensheni tumekubaliana
tutaweka nguvu kwa pamoja kuhakikisha miradi yote kumi (10) iliyobuniwa na
TAFICO inayoangazia kutengeneza mazingira thabiti ya uvuvi inasimama kwa awamu
nyingine tena ili tija ya shirika hilo iweze kuonekana,” alisisitiza Justine.
Naye, Katibu Mkuu, Wizara
ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah alisema kuwa uendeshaji wa shirika
hilo kwa awamu hii utakuwa ni wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi.
Aliongeza kuwa kwa miaka
mingi tangu uhuru haukuwepo uwekezaji katika bahari kuu huku akisema kuwa ni
mategemeo yao kuwa uwekezaji ukianza katika uvuvi wa bahari kuu samaki wataongezeka
mara tatu zaidi ya wanaopatikana sasa.
Dkt. Tamatamah alisema kuwa
shirika hilo likianza kufanya kazi sekta ya uvuvi itaimarika na pia litasaidia
kuzuia uvuvi haramu na kulinda rasilimali za uvuvi katika bahari kuu.
Taasisi zilizoshiriki kikao
hicho ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Benki ya CRDB, Benki ya NMB, na
Benki ya Posta (TPB).
Nyengine ni Kituo cha
Uwekezaji, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Hifadhi ya
Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).