Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Makungu akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati.
……………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Manyara
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU imewapa onyo Wenyeviti wa vijiji kutouza ardhi kiholela na kutambua kuwa sheria ya ardhi ya vijiji haziwapi mamlaka wenyeviti wa mitaa, vitongoji na vijiji kuuza ardhi bila ridhaa ya mkutano mkuu.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph ameyasema hayo mjini Babati wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Makungu ameyasema hayo baada ya baadhi ya wenyeviti wa vijiji vitongoji na mitaa mkoani humo kuuza ardhi kinyume na taratibu na kusababisha migogoro katika maeneo hayo.
Amewaambia wananchi kuwa mamlaka ya kuuza ardhi kwa maana ya ardhi ya kijiji yapo mikononi mwa mkutano mkuu wa kijiji kwa ekari 50 na kushuhudia mauziano kwa mujibu wa sheria hizo yapo kwa ofisi ya watendaji na sio wenyeviti.
“Kwa msingi huo mauziano yanayofanywa kupitia wenyeviti ni batili na hayana nguvu ya kisheria, hivyo wananchi wawe waangalifu na vitendo vya baadhi ya wenyeviti wachache wasio waadilifu wanaojihusisha na uuzaji wa ardhi,” amesema Makungu.
Pia, Makungu amesema katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba mwaka huu TAKUKURU mkoa wa Manyara imepokea malalamiko 208 ambapo kati ya hayo 127 yalihusiana na makosa ya rushwa na malalamiko 81 yalihusu makosa mengine ambapo walalamikaji walishauriwa na kuelekezwa katika ofisi husika kwa ajili ya utatuzi wa malalamiko yao.
Amesema kesi mbili zilizokamilika watuhumiwa wote walikutwa na hatia huku kesi mbili mpya zikiendelea mahakamani.
“Natoa rai kuwa sheria ziendelee kufuatwa kwani mtu yeyote ambaye hatafuata atachukuliwa hatua kali za kisheria na kufikishwa mahakamani,” amesema Makungu.