*********************************************
NA EMMANUEL MBATILO
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya inawashikiria watuhumiwa watatu kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya heroin.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya James Kaji amesema watuhumiwa hao ni Anadhati Rashid Mchongeza mwenye umri wa miaka 20, Emmanuel Msakuzi umri miaka 23 na Kulwa Pazi Shamas umri miaka 49 ambaye anafahamika zaidi kwa jina la udodi ambaye pia ni balozi wa nyumba 50 katika mtaa wa Juwaje Kunduchi Pwani.
“Watuhumiwa walikamatwa tarehe 22 Januari, 2021 katika eneo la Kunduchi Pwani Kauzeni Jijini Dar es Salaam wakiwa na unga unaodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya Heroin kiasi cha gram 400 na majani makavu ya bangi puli moja (kiasi hicho ni sawa na kete 30 za bangi)”. Amesema Kamishna Jenerali Kaji.
Aidha Kamishna Jenerali Kaji amesema Mamlaka hiyo inaendelea kuwashikilia watuhumiwa na watafikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria kukamilika.
Pamoja na hayo Kamishna Jenerali Kanji amesema wataendelea kutoa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya kwa njia mbalimbali ikiwemo matukio makubwa ya kitaifa na vyombo vya habari.
“Mamlaka imeandaa mwaongozo wa uelimishaji wa wadau wanaofanya uelimishaji kwa makundi mbalimbali ya kijamii unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu wa fedha”. Ameongeza Kamishna Jenerali Kanji.