…………………………………………………………………………………
Na MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
KITUO cha afya MEDWELL kilichoko halmashauri ya mji Kibaha ,mkoani Pwani kimetoa huduma bure za upasuaji wa mtoto wa jicho kwa zaidi ya wagonjwa elfu mbili ,katika kipindi cha mwaka jana na mwaka huu mwezi januari 2021.
Pamoja na upasuaji huo wa mtoto wa JIcho , pia kituo hicho kimeendesha zoezi maalumu la kutoa matibabu bure na upimaji wa magonjwa ya akina mama ikiwa ni pamoja na upimaji wa saratani ya mlango wa shingo ya kizazi.
Mkurugenzi mkuu wa kituo hicho Bashiru Khaki, anasema kambi hiyo ni ya siku mbili ambapo walilenga kuhudumia wakina mama na jamii.
“Wingi wa wakinamama waliojitokeza kupata vipimo na matibabu baada ya kutangaziwa kuna huduma hii ya bila malipo limeonyesha picha kuwa kuna uhitaji mkubwa wa huduma za afya, hivyo tunajipanga kutoa huduma hizi mara kwa mara ili wananchi wawe na afya njema na waweze kufanya kazi na kuinua uchumi wa nchi, alisema, Khaki
Kwa upande wa huduma ya macho pamoja na upasuaji wa mtoto wa Jicho, mkurugenzi huyo alisema huduma hiyo hutolewa kila siku ya jumanne na ijumaa na kuwa siku zote hutolewa bure.
Amina Ramadhani ni meneja rasilimali watu, anasema zoezi hilo lilipangwa kufanyika kwa muda wa siku moja lakini kutokana na wingi wa wagonjwa litafanyika Siku mbili , jumamos na jumapili.
” Medwel tumejikita zaidi kuhudumia jamii hususani katika suala zima la afya, hapa tunatoa huduma za vipimo mbalimbali ,xray na ultrasound, pia upasuaji , huduma za kulaza wagonjwa na nyingine nyingi, pia tunachimba visima na hata katika suala la elimu pia tunachangia, lengo ni kuisaidia serikali yetu katika kuimarisha afya ya wananchi wake,” alisema Amina
Mganga mkuu wa mkoa wa Pwani Dr. Gunini Kamba ,alipongeza kituo hicho kwa jinsi kinavyounga mkono juhudi za serikali katika suala la afya kwa wananchi wake na kuwa serikali itaendelea kushirikiana nao pia akavitaka wadau wengine wa afya wajitokeze kufanya huduma kama hizo.