…………………………………………………………………
Na Bryson Mshana, Mtwara
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele Mtwara, imeanza kuunga Mkono kwa vitendo kampeni ya kuhamasisha upandaji wa mikorosho ijulikanayo kama “ondoa mapori ongeza uzalishaji” yenye lengo la kuongeza uzalishaji wa wa zao la Korosho katika Mkoa wa Mtwara.
Katika kutekeleza hilo, hii leo Januari 25, 2021 TARI Naliendele imeendesha zoezi la uondoaji wa Mikorosho ya zamani sambamba na utoaji wa elimu ya upandaji na utunzani wa Mikorosho, katika Shamba la shue ya Msingi Naliendele iliyopo Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Zoezi hilo limehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya, ambaye ameupongeza uamuzi huo wa TARI, huku akiishauri Tasisi hiyo ya utafiti wa Kilimo kuzifikia Shule nyingine zaidi na kaunzisha mashamba darasa kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu uzalishaji wa zao la Korosho.
DC Kyobya pia amewaagiza watendaji Kata na Maofisa Tarafa za Wilaya ya Mtwara, kufuatilia upatikanaji wa mashamba kwa ajili ya shule zingine ili ziingie kwenye kilimo cha Korosho jambo ambalo litaongeza uzalishaji kupitia mashamba ya shule.
Pamoja na zao la Korosho, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi, wakuu wa Shule na watendaji wengine kuangalia namna ya kulima mazao mengine mbadala kwenye mashamba yao ya mikorosho kwa kuzingatia elimu watakayokuwa wakipewa na wataalam wa TARI.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa TARI Naliendele Dr. Fortunatus Kapinga, emeeleza kuwa wamekuwa na uhusiano wa karibu na Shule ya Msingi Naliendele tangu Mwaka 1999, katika kuhakikisha kuwa wanatoa elimu ya uzalishaji wa Korosho kwa Wanafunzi pamoja na Wananchi maeneo ya jirani.
Dr. Kapinga amesema zoezi lililoanza leo litasaidia kuondoa mikorosho ya zamani, kupanda na kupandikiza mipya, kufanyia usafi shamba pamoja na kuendelea kutoa ushauri ili kuhakikisha kwamba azma ya kuongeza uzalishaji inafikiwa.
Awali akisoma taarifa fupi kwa Mkuu wa Wilaya, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Naliendele Bi. Dionita George ameishukuru TARI kwa juhudi ambazo imekuwa ikizifanya katika kuhakikisha kwamba Shamba la Shule hiyo linazalisha Korosho kwa Wingi.
Bi. Dionita ameeleza kuwa kupitia uwezeshwaji wa TARI wamekuwa wakivuna Korosho bora na kuziuza kwa bei nzuri, hivyo kupata fedha za kutatua changamoto mbalimbali shuleni hapo ikiwa ni pamoja na ukarabati wa miundombinu ya shule.
Ameongeza kuwa Mafanikio hayo yaliyotokana na uwepo wa Shamba la mikorosho, yamesaidia kupunguzia wazazi mzigo wa michango kwa watoto wanaosoma shuleni hapo huku akielezwa kuwa mwaka 2017 shule iliweza kuweka umeme Nyumba tatu za waalimu,kujenga jiko la muda kwa ajili ya kupikia huku mwaka 2019 wakijenga maboma mawili ya madarasa ikiwa ni sehemu ya mafanikio ya uwepo wa Shamba la mikorosho shuleni hapo.
Disemba 16, 2020 Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa, alizindua rasmi kampeni ya kuhamasisha upandaji wa mikorosho mipya yenye lengo la kuongeza uzalishaji wa zao la Korosho katika Mkoa wa Mtwara.
Kampeni hiyo aliyoipa jina la “ondoa mapori ongeza uzalishaji” ilizinduliwa Wilayani Mkoani Mtwara, ikilenga kutoa elimu ya kuongeza uzalishaji kwa wakulima wa Korosho waweze kufufua mapori, kuondoa mikorosho iliyozeeka na kulima kisasa kwa ajili ya kupata mavuno yenye tija.